Mgogoro DRC waongeza ugumu wa maisha

Vibanda vya wafanyabiashara wa sarafu katika soko la 'Kintambo Magasin' lililoko katika jiji la Kinshasa. Picha na Arsene MPIANA / AFP

Kushuka kwa sarafu ya ndani, malimbikizo ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na matumizi ya vita kumeongeza bei za bidhaa katika nchi maskini ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuwaacha wakongo wakihangaika kumudu mahitaji ya msingi.

Tangu mwaka mpya, faranga ya Kongo imeshuka thamani kwa takriban asilimia 15 dhidi ya dola ya Marekani, kulingana na takwimu rasmi na wabadilisha fedha, na kuwaathiri sana watu wenye kipato cha chini.

Watu kadhaa waliohojiwa na shirika la habari la AFP walisema kuwa wakati mwingine bei hupanda juu sana, mara mbili au zaidi.

Kupanda kwa bei za bidhaa kunatokana na kuongezeka kwa matumizi ya serikali katika mapambano dhidi ya kundi la waasi la M23 -- ambalo limeteka maeneo mengi yaliyoko mashariki mwa Kongo tangu mwaka jana.

Mchumi mmoja, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kuwa matumizi ya serikali yameelekezwa katika uagizaji bidhaa kutoka nje huenda zinahusiana na mzozo, pia kuhusu malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi wa umma.

Ukiongeza mfumuko wa bei duniani na uchumi unaotegemea uagizaji bidhaa kutoka nje na dola za Marekani, raia wengi wa Kongo wanahisi machungu.

Akiwa amesimama kwenye matope katika soko lililoko katika mji mkuu wa Kinshasa, Bibiche Musabili alikuwa ameshika majani ya viazi vitamu -- chakula kikuu kinachotumiwa na wenyeji inayojulikana kama Matembele.

"Tulikuwa tukinunua hii mboga kwa faranga 500, sasa imeongezka bei na imekuwa faranga 3,000," alisema mwanamke huyo.

"Tutafanya nini?" aliongeza Musabili, ambaye alisema watoto wake hawana chakula.

Takriban theluthi mbili ya watu milioni 100 ya wakazi wa DRC wanaishi chini ya dola 2.10 kwa siku, kulingana na Benki ya Dunia

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP