Meya Buttigieg ajitoa katika mbio za kuwania urais wa Marekani 2020

Meya wa zamani Pete Buttigieg

Meya wa zamani wa South Bend, Indiana, Pete Buttigieg amamua kujitoa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Marekani 2020.

Kampeni ya Buttigieg ilitangaza Jumapili jioni kuwa mgombea wao ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya nne ambapo hakupata wajumbe wowote.

Wakati huo huo Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden, aliyeshinda kwa kishindo uchaguzi wa chama hicho South Carolina, anakabiliwa na changamoto mpya kutoka kwa Seneta wa Vermont Bernie Sanders wakati majimbo 14 yatakapopiga kura Jumanne katika mashindano ya chama kote nchini Marekani.

Biden, alikuwa hajawahi kushinda kwenye jimbo lolote katika uchaguzi huo wa awali wa urais mara tatu hadi mafanikio hayo ya Jumamosi.

Lakini utafiti wa maoni kabla ya uchaguzi unaonyesha kwamba Sanders, mwenye mrengo wa kushoto wa kisoshalisti aliyejitangaza kugombea kupitia chama cha Demokratic, anaongoza kwa kiasi kikubwa huko California.

Inatarajiwa kuwa atakuwa na kuna kura nyingi za wajumbe wa mkutano mkuu ujao wa kitaifa wa uteuzi wa mgombea wa chama cha Demokrat katika msimu wa joto katika duru ijayo ya kupiga kura.