Wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran wamerusha dazani za makombora kwa wiki kadhaa sasa, zikilenga meli zinazopita katika eneo hilo, lakini bila ya kusababisha uharibifu mkubwa, au mara nyinginge, hata kukosa shabaha zao, juhudi zinazolenga kujaribu kuilazimisha Israel kuachana na vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas kwenye ukanda wa Gaza.
Lakini shambulio la hivi punde lilikuwa moja yale mabaya zaidi kuwahi kufanyika. Kamandi kuu ya jeshi la Marekani ilisema kuwa moja ya meli zake za kivita, pamoja na meli nyingine ya kibiashara, zilienda karibu na eneo la tukio na kusaidia kuwapeleka wafanyakazi wa meli iliyoathiriwa, hadi kwenye bandari salama iliyo karibu.
Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi Yahya Sarea alisema katika taarifa yake kwamba wanamgambo walishambulia meli ya Rubymar, kuiharibu vibaya, na kuiacha "katika hatari ya kuzama."
Hapo awali Wahouthi walisema wiki zilizopita walikuwa wakishambulia meli zinazomilikiwa na Waisraeli au zinazosafiri kwenda na kutoka bandari za Israeli, lakini tangu wakati huo wamekuwa wakilenga meli zisizohusiana na Israeli, na zinazoelekea maeneo mengine.