Gavana wa Michigan Gretchen Whitmer mwishoni mwa wiki amepiga marufuku kula ndani ya migahawa, kwenda shule na vyuoni, matukio ya umma pamoja na mikusanyiko kwenye casino na majumba ya sinema.
Mikusanyiko ya nyumbani haitaruhusiwa zaidi ya watu 10 kwa wakati mmoja. Kwenye jimbo la kaskazini magharibi la Washington, Gavana Jay Inslee pia amepiga marufuku ulaji wa ndani ya migahawa huku akiamuru maduka ya reja reja kuruhusu asilimia 25 pekee ya wateja kwa wakati mmoja.
Mikusanyiko ya nje isivuke watu watano huku mikusanyiko ya ndani ya nyumba ikiruhusiwa wanafamilia pekee.
Katika kipindi cha wiki moja iliopita, Marekani imekuwa ikitangaza karibu visa 150,000 vya maambukizi mapya kwa siku kulingana na takwimu zilizotolewa na chuo kikuu cha Johns Hopkins.
Zaidi ya watu 246,000 hapa Marekani tayari wamekufa kutokana na janga hilo tangu lilipoingia mwanzoni mwa mwaka.