Katika taarifa, wizara ya fedha ya Marekani ilisema watu hao ni pamoja na afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Kongo na mmoja wa Rwanda, na wanachama wanne waandamizi wa makundi ya waasi yenye silaha, ambayo yamekuwa yakisababisha hali ya taharuki kwenye mipaka ya mashariki mwa Kongo kwa miongo kadhaa.
Kundi linaloungwa mkono na Rwanda la M23 liliteka baadhi ya maeneo ya jimbo la Kivu Kaskazini mwezi Novemba 2021, na kuzidisha mapigano na wanajeshi wa Kongo na wanamgambo wengine ambao wamesababisha maelfu ya raia kupoteza makazi yao.
"Vikwazo vya leo vinaonyesha kujitolea kwa Marekani katika kuendeleza juhudi za kutatua mgogoro huo na kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu," Brian Nelson, waziri mdogo fedha anayeshughulika na masuala ya ugaidi na ujasusi wa kifedha, alisema katika taarifa hiyo.
"Pande zote katika mzozo zinawajibika kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na, lakini sio tu, kuwalenga kimakusudi raia kupitia unyanyasaji wa kijinsia," alisema.
Mapigano na majanga ya asili yanayotokea mara kwa mara yamechochea mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa Kongo. Takriban watu milioni 5.5 wamekimbia makazi yao katika Kivu Kaskazini na majimbo jirani, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.