Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 19:39

DRC: Kikosi cha Afrika mashariki kuanzisha uchunguzi kuhusu mauaji yanayodaiwa kufanywa na M23


Mwanajeshi wa M23 akilinda eneo la mkutano kati ya maafisa wa kikosi cha Afrika mashariki na waasi wa M23 wakati wa hafla ya kukabidhi kambi ya Rumangabo kwa wanajeshi wa Afrika mashariki, Januari 6, 2023.
Mwanajeshi wa M23 akilinda eneo la mkutano kati ya maafisa wa kikosi cha Afrika mashariki na waasi wa M23 wakati wa hafla ya kukabidhi kambi ya Rumangabo kwa wanajeshi wa Afrika mashariki, Januari 6, 2023.

Kikosi cha Afrika Mashariki kinachosimamia juhudi za kutafuta amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumatatu kimesema kitatuma tume ya uchunguzi katika eneo ambako wakazi waliwashutumu waasi wa M23 kuua watu 11.

Kundi la M23 limekanusha kufanya mauaji hayo.

Lakini kwa mujibu wa vyanzo katika eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini, miili ya watu 11 ambao walipigwa risasi au kukatwakwatwa hadi kufa ilipatikana siku ya Jumapili.

Vyanzo hivyo vilisema miili hiyo ilipatikana katika kijiji cha Bukombo, kwenye umbali wa kilomita 100 kaskazini mwa mji wa Goma, baada ya waasi wa M23 kuondoka katika eneo hilo.

Taasisi inayofuatilia masuala ya usalama nchini DRC, Kivu Security Tracker (KST), Jumatatu ilisema kwamba raia 11 waliuawa katika eneo hilo baada ya kulazimishwa kusafirisha zana za kijeshi.

Iliongeza kuwa kundi la M23 ndilo linashukiwa kwa mauaji hayo. Lakini msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka alikanusha kuhusika kwa kundi lao.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba M23 walikabidhi udhibiti wa eneo la Bukombo kwa kikosi cha wanajeshi wa Jumuia ya Afrika mashariki kilichopelekwa mashariki mwa DRC.

Forum

XS
SM
MD
LG