Marekani na Ujerumani kuongoza mjadala wa hali ya dharura ya Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken wakihutubia mkutano wa waandishi wa habari Berlin, 23.06.2021.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ni wenyeji wa mazungumzo Jumatano na kundi la washirika na wadau kujadili hali nchini Afghanistan.

Mkutano huo pia utajadili pamoja na juhudi za kuendelea kupeleka misaada ya kibinadamu kwa nchi hiyo ya Afghanistan baada ya Taliban kuchukua Madaraka.

Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema kabla ya mkutano wa mawaziri kwamba moja ya mada ya majadiliano itakuwa kuona iwapo Taliban watatimiza ahadi zao na kutekeleza matarajio ya jumuiya ya kimataifa.

Kabla ya kusafiri kwenda Ujerumani, Blinken alisisitiza wakati wa ziara yake Qatar kwamba Marekani na wengine wanatoa wito kwa Taliban kutimiza ahadi zao za kuruhusu mtu yeyote mwenye hati halali za kusafiria aondoke Afghanistan ikiwa atachagua kufanya hivyo.

Suala hilo limelengwa tangu Marekani ilipojiondoa kutoka Afghanistan mwishoni mwa Agosti, ikimaliza miongo miwili ya uwepo wa jeshi la Marekani na juhudi ya mwisho ya kuwaondoa maelfu ya watu kutoka nchi hiyo.

Watu wengi ambao walitaka kuondoka Afghanistan hawakuweza kufanya hivyo kabla ya kujiondoa kwa Marekani.