Mashuhuda wamesema kwamba, jeshi lilianzisha mashambulizi ya anga na mizinga mikubwa, na kulikuwa na mapigano ya ardhini katika maeneo kadhaa ya Omdurma.
RSF ilisema Jumatatu kwamba iliidungua ndege ya kivita, na wakaazi walichapisha picha zilizokuwa zikionyesha marubani wakitoka kwenye ndege.
Mzozo kati ya jeshi na Wanajeshi wa kikosi cha dharula (RSF) ulianza tarehe 15 Aprili, na kusababisha mapigano kila siku katika mji huo mkuu, pamoja na mauaji ya kikabila katika jimbo la magharibi la Darfur, na kutishia Sudan kuingia katika vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe.
Wakazi wa maeneo ya mji huo walisema mapigano ya Jumanne katika mitaa ya Omdurman yalikuwa makali kushinda yote yaliyotokea katika wiki zilizopita, na kwamba wakati jeshi lilipokuwa likijaribu kuongeza nguvu pia lilikuwa likijihami dhidi ya shambulio la RSF katika kambi ya polisi.
"Kumekuwa na mashambulizi makubwa kwa muda mrefu, mashambulizi ya anga, mizinga na risasi. Ni mara ya kwanza tumekuwa katika mashambulizi ya mfululizo yaliyofanywa na pande zote ," alisema Manahel Abbas, mwenye umri wa miaka 33 mkazi kitongoji cha Al-Thawra kilichopo Omdurman.
Mzozo huo ulizuka kutokana na mpango ulioungwa mkono na Jumuia ya Kimataifa kwa ajili ya kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia, miaka minne baada ya kupinduliwa kwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir wakati wa uasi wa wananchi.
Saudi Arabia na Marekani zilipendekeza makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano wakati wa mazungumzo ya Jeddah ambayo yalisitishwa mwezi uliopita baada ya pande zote mbili kukiuka makubaliano hayo.
Takriban watu milioni 2.8 wamekimbia makazi yao tangu mapigano yazuke katikati ya mwezi wa Aprili, mapigano ambayo pia yamesababisha takriban watu 650,000 kukimbilia nchi jirani, kulingana na takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters