Mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya yathibitisha hakuna aliyeathiriwa na dawa ya Fentanyl

Mkurugenzi wa Taasisi ya Reachout Centre Trust Taib Abdulrahman (wakwanza kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa NACADA, John Muteti (wapili kulia).

Mamlaka ya kitaifa ya kupambana na dawa za kulevya Kenya, NACADA, imesema hakuna kesi yoyote ya dawa ya Fentanyl kama ilivyodhaniwa.

Ripoti ya mamlaka ya NACADA, imejiri baada ya video kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu wakiwa wamelegea na kuduwaa, mwezi mmoja uliopita.

Afisa mkuu wa mamlaka hiyo John Muteti, ameeleza kuwa uchunguzi wao wa sampuli za damu 20 zilizofanyiwa utafiti katika maabara ya serikali, umegundua kwamba hakuna kilichobainika kuhusu kuwepo kwa dawa hiyo ambayo mtu anayetumia hulegea.

"Sababu nyingine huenda ikawa mchanganyiko wa heroin na Xylazine, dawa inayotumika kuwalaza mifugo wakati wakitibiwa, hii ni hatari kwa afya ya umma na kuna haja ya kuwepo kwa hatua za haraka kudhibiti usambazaji wa dawa kuingia katika biashara haramu,” asema Muteti.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Reachout Centre Trust, shirika la kurekebisha waathirika wa dawa za kulevya, Taib Abdulrahman, akisema kuwa dawa hiyo haipo nchini kwani ingezua madhara mengi ikiwemo yale ya kutumia dawa hizo kupita kiwango, hali ambayo ingesababisha hata vifo miongoni mwa waraibu.

“Jambo moja kubwa katika hizi zinazotolewa tiba yake ni tofauti lazima tujue tutatumia tiba gani? Tukipata watu wanatumia dawa za kwenye mabox ‘over the counter’ itakuwa hatari kubwa sana. Cha kushukuru hatukupata kesi ya overdose.” Taib Abdulrahman amesema.

Mwenyekiti wa mamlaka ya NACADA Stephen Mairori, amewaonya walanguzi wa dawa za kulevya, watafute biashara halali ambazo hazitaathiri afya ya binadamu.

Idara ya usalama ikitoa onyo kwa wanaouza dawa hizo kiholela huku ikiihimiza jamii kushirikiana na vitengo vya usalama katika kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya.

“Ni jukumu la vitengo vyote vya usalama kupiga vita matumizi ya mihadarati kwani hali hii inaweza kuwaingiza vijana katika magenge ya uhalifu.” Rhoda Onyancha, mkuu wa usalama pwani ya Kenya.

Mwenyekiti anasema kukosekana kwa heroine huenda kumechangia waraibu kutafuta mchanganyiko wa dawa mbali mbali bila ya kujali madhara yake.