Mamilioni hatarini kufa kwa kutofikiwa na misaada ya kibinadamu huko Gaza

Vifaru vya Israel vikiwa kazini wakati mzozo kati ya Israel na Hamas ukiendelea huko Gaza Januari 8, 2024. Picha na REUTERS/Ronen Zvulun

Shirika la Afya Duniani linaonya kuwa mamilioni ya watu waliojikuta katika mgogoro unaosababisha dharura za kiafya, wako hatarini kufa kutokana na majeraha na magonjwa ya kuambukiza kwa sababu ya kutofikiwa na misaada ya kibinadamu inayohitajika.

Katika moja ya hoja zake zenye nguvu zaidi kuliko zote, mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameishutumu serikali ya Israel kwa kuzuia misaada muhimu inayokwenda Gaza.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumatano, Tedros amesema misaada ya kibinadamu kwenda kaskazini mwa Gaza iliyopangwa siku hiyo ya sita tangu Desemba 26, ilibidi ifutwe kwa sababu “maombi yetu yalikataliwa na uhakika wa usalama wa kupitisha haukutolewa.

Usambazaji misaada ya kibinadamu huko Gaza unaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi. Mashambulizi makali ya mabomu, masharti ya kutembea, uhaba wa mafuta na mawasiliano mabaya yanafanya iwe vigumu kwa WHO na washirika kuwafikia wale wanaoihitaji misaada” alisema.

Maafisa wa WHO wamesema Gaza inajiandaa na kile wanachokiita dhoruba kamili ya kusambaa kwa magonjwa. Ilipofika Januari Mosi, watu taribani 200,000 wameorodheshwa wana magonjwa ya kuambukiza na maelfu ya visa vya watu wenye chawa, magonjwa ya ngozi, na homa ya manjano.

Shirika hilo limesema limeorodhesha visa 2,140 vya magonjwa ya kuharisha kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kati ya mwaka 2021 na 2022; ilipofika Novemba 2023, idadi hiyo iliongezeka mara 20 na kufikia visa 42,655