Mama ya Navalny aomba Putin amsaidie kupata mwili wa mwanawe

  • VOA News

Mama ya Alexei Navalny, Lyudmila Navalnaya.

Mama wa marehemu kiongozi wa upinzani wa Russia Alexey Navalny Jumanne, ameomba Rais Vladimir Putin aingilie kati na kuachilia mwili wa mwanawe, ili aweze kuuzika kwa njia ya heshima.

Lyudmila Navalnaya wakati akiwa amevalia mavazi meusi ameonekana kwenye video akiwa nje ya jela lilipo Arctic, ambako Navalny alifia Ijumaa iliopita, akiwa na umri wa miaka 47. “Kwa siku ya 5, sijaweza kumuona ,” amesema Navalnaya, akiongeza kuwa wamekataa kuachiliwa mwili wake, na wala hawamwambii alipo.

Timu ya Navalny imesema kwamba serikali ya Russia imesema kwamba kiini cha kifo chake hakijulikani, wakati ikiendelea kushikilia mwili wake kwa muda wa wiki mbili, ili kutoa muda kwa uchunguzi kufanyika. Timu hiyo pia imedai kuwa serikali inavuta muda, ili kujaribu kuficha ushahidi kwamba aliuwawa.

Jumatatu mjane wa Navalny, Yulia alitoa video akimlaumu Putin kwa mauaji hayo, akidai kuwa kukataa kuachilia mwili wake ni moja wapo ya mbinu za kujaribu kuficha ukweli.