Akizungumza katika tukiohuko Afrika Kusini, Yousafzai alitoa wito kwa dunia kuitaka izingatie kile kinachowatokea wasichana na wanawake wanaoishi chini ya utawala wa Taliban nchini Afghanistan.
Malala Yousafzai, mwanaharakati wa Pakistani ambaye alinusurika baada ya kupigwa risasi kichwani na wanachama wa Taliban waliokuwa na silaha alipokuwa na umri wa miaka 15 kwa kuthubutu kutaka kuendelea na masomo, alitoa hotuba ya kila mwaka ya Wakfu wa Nelson Mandela huko Afrika Kusini Jumanne, hotuba ambayo mwaka huu iliadhimisha miaka kumi tangu kifo cha rais huyo wa kwanza wa Afrika Kusini aliyechaguliwa na wananchi.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka ishirini na sita alionyesha uwiano kati ya mapambano ya muda mrefu ya Mandela dhidi ya utawala wa wazungu wachache na ubaguzi wa rangi wakati wa utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini na hali ambayo wanawake wa Afghanistan wanakabiliana nayo katika kipindi cha miaka miwili tangu utawala wa Taliban kurejea madarakani.
"Nikiwa na mawazo ya urithi wa Mandela, nilijiuliza: Je, ni ukosefu gani wa haki ambao dunia haiuangalii? Je, ni wapi tunaruhusu unyama kuwa na nafasi? Kwangu jibu lilikuwa wazi kabisa, na la binafsi sana: ukandamizaji wa wasichana na wanawake Afghanistan,” alisema.
Yousafzai, ambaye alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel akiwa na umri wa miaka 17 tu, aliishutumu kile kilichopo, kwamba migogoro mingine inavuta hisia za dunia na kuacha kuiangalia hali iliyoko Afghanistan, ambako wasichana hawaruhusiwi kuhudhuria shule za sekondari na wanawake wamepigwa marufuku kufanya kazi au hata kutoka nje ya nyumba zao wenyewe.
"Waafrika Kusini walipambana ili ubaguzi wa rangi utambuliwe na kuharamishwa katika ngazi ya kimataifa ... Lakini ubaguzi wa kijinsia bado haujapewa nafasi. Ndiyo maana natoa wito kwa kila serikali, kila nchi, kuufanya ubaguzi wa kijinsia kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu,” alisema.
Mjane wa Mandela, na mtetezi wa haki za wanawake, Graca Machel, pia alizungumza katika hafla hiyo.
"Hebu tuseme ukweli, hiki kitu cha wanaume kufikiria kuwa wana haki juu ya maisha ya wanawake, hiki kitu ambacho kwao wanaamini kuwa wana haki juu ya miili ya wanawake, lazima sasa kikomeshwe!" alisema Machel.
Mshindi huyo wa tuzo ya Amani ya Nobel pia alisema Umoja wa Mataifa unapaswa kupitisha lugha inayohusu ubaguzi wa kijinsia katika rasimu mpya wanayoiandika kuhusu Uhalifu dhidi ya Ubinadamu.