Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ya Marekani ya District of Columbia Circuit ilitupilia mbali madai ya Trump kwamba hawezi kushtakiwa kwa sababu madai hayo yanahusiana na majukumu yake rasmi alipokuwa rais.
Uamuzi huo, ambao bila shaka Trump atakata rufaa, unatupilia mbali jaribio lake la kuepuka kesi kwa mashtaka ya kuwa alihujumu demokrasia ya Marekani na makabidhiano ya madaraka, licha ya kuendelea kujizatiti katika nafasi yake kama mgombea wa mbele wa uteuzi wa nafasi ya urais kwa chama cha Republikan.
Mawakili wa Trump wametoa hoja kuwa marais wa zamani wanastahili kupewa kinga ya kisheria ya jumla na hawawezi kufunguliwa mashtaka ya uhalifu kwa hatua rasmi walizochukua ila kwanza wawe wamefunguliwa mashtaka na Baraza la Wawakilishi na kuondolewa katika wadhifa wao na Baraza la Seneti.
Trump alifunguliwa mashtaka mara mbili na Baraza la Wawakilishi, lakini kila wakati Baraza la Seneti lilipiga kura za kutosha kumuondolea mashtaka yanayomkabili.