Mahakama ya Juu India yatupilia mbali ombi la kuachiliwa mapema wabakaji 11

Wanawake India wakiandamana kulaani vitendo vya ubakaji na kusema kupitia mabango yao kitendo cha kuwaachilia mapema wabakaji ni uhalifu wa kinyama.

Mahakama ya Juu India Jumatatu imetupilia mbali ombi la kuachiliwa mapema kwa wanaume wa Kihindu 11 ambao wanatumikia kifungo cha maisha kwa kushiriki katika ubakaji wa genge dhidi ya mwanamke wa Kiislam aliyekuwa mjamzito.

Watu hao pia waliwaua ndugu za mwanamke huyo wa Kiislam wakati wa ghasia baina ya Wahindu na Waislam katika jimbo la Gujarat mwaka 2002, wakili mmoja katika kesi hiyo alisema.

Mahakama hiyo ilielekeza wanaume hao kujisalimisha kwa mamlaka ya gereza katika kipindi cha wiki mbili, wakili huyo aliongeza.

Muathirika huyo, Bilkis Bano, alikuwa na mimba ya miezi mitatu wakati alipobakwa na kikundi hicho cha wabakaji na ndugu zake kadhaa, akiwemo mtoto wake wa miaka mitatu, kuuwawa wakati wa ghasia hizo zilizotapakaa kote katika jimbo hilo, likiuwa zaidi ya watu 1,000, wengi wao Waislam.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi

Waziri Mkuu Narendra Modi alikuwa wakati huo waziri kiongozi wa Gujarat na Chama chake cha Hindu cha Bharatiya Janata bado kinatawala katika jimbo hilo.

Wanaume hao waliohukumiwa mapema mwaka 2008, waliamriwa waachiliwe huru na serikali ya Gujarat Agosti 2022 baada ya gereza waliokuwa wanashikiliwa kutoa pendekezo waachiliwe ikizingatia muda waliokuwa wametumikia kifungo na mwenendo wao mzuri.

Kuachiliwa kwao kulilaaniwa na mume wa muathirika, mawakili na wanasiasa. Vyombo vya habari vya eneo viliripoti rufaa kadhaa zilizofunguliwa katika Mahakama ya Juu vikipinga kupunguzwa kifungo hicho, ikiwemo moja iliyofunguliwa na muathirika mwenyewe.

Katika uamuzi wake Jumatatu, mahakama hiyo ilisema kuwa Gujarat haina mamlaka ya kupunguza adhabu iliyotolewa kwa vile kesi hiyo ilihamishiwa Mumbai, na kulifanya jimbo jirani la Maharashtra kuwa na jukumu kwa uamuzi huo.

“Mahakama hiyo ilisema kuwa sheria iko wazi, serikali husika ni serikali ambako waliotuhumiwa kesi yao ilisikilizwa na hukumu kutolewa,” wakili Vrinda Grover, kati ya mawakili waliowakilisha rufaa, aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.