Kiongozi wa kijeshi wa Chad amesema ataheshimu matokeo ya uamuzi, ambao kuna uwezekano mkubwa hayatatofautiana na matokeo ya majimbo yaliyotolewa siku ya Jumapili yanayoonyesha asilimia 86 ya wapigakura wameidhinisha katiba mpya ya nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Baadhi ya viongozi wa upinzani walitoa changamoto kwa utawala wa kijeshi, wakisema katiba iliyopitishwa katika kura ya maoni haitoi uhakikisho kuwa viongozi wa kijeshi wako tayari kukabidhi madaraka kwa raia.
Serikali ya mpito ya kijeshi ya Chad imesema, idadi ya kubwa ya wapiga katika kura ya maoni ya katiba ya nchi hiyo inaonyesha kiwango kikubwa cha watu wanakubaliana na mpango wa jenerali Mahamat Idriss Deby wa kukabidhi mamlaka kwa raia ifikapo Mwezi Desemba 2024.
Deby alizungumza kupitia kituo cha televisheni ya taifa wiki hii baada ya matokeo ya awali kwa kura ya maoni kutangazwa.
Kulingana na matokeo ya awali, katiba mpya imeidhinishwa na asilimia 86 ya wapiga kura.
Lakini viongozi wa upinzani nchini Chad na makundi ya kiraia wanasema idadi kubwa ya wapigakura hawakujitokeza kupiga kura.