Macron akutana na maafisa wa serikali kujadili uchunguzi kuhusu machafuko

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron awahutubia mameya takriban 300 kufuatia maandamano yaliyosababishwa na kuuawa kwa kijana mmoja ambayo yalizua vurugu. Julai 4, 2023. (Picha na Ludovic MARIN )

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Jumanne alikutana na mamia ya maafisa wa Ufaransa, ukiwa ndio mwanzo wa uchunguzi wa kile alichokiita  "sababu za kina" za nchi hiyo kutumbukia katika machafuko, baada ya mauaji ya kijana mmoja ambaye gari lake lilikuwa limesimamishwa na afisa wa polisi.

Mkutano huo katika ikulu mjini Paris, ulihudhuriwa na zaidi ya mameya 300, ambao manispaa zao, zilishuhudia uharibifu kutokana na wiki ilyojaa vurugu, na ulifanyika baada ya mamlaka kuripoti usiku wa utulivu nchini kote.

"Sote tunataka utaratibu wa kudumu. Hicho ndicho kipaumbele kikuu," alisema Macron.

Serikali ya Macron imepambana na ghasia na uporaji tangu Nahel M., mwenye umri wa miaka 17, kuuawa na afisa mmoja hapo tarehe 27, mwezi jana, nje kidogo ya jiji la Paris, na kuibua tena shutuma za muda mrefu, za ubaguzi wa rangi, miongoni mwa vikosi vya usalama.

Ghasia za usiku katika miji ya Ufaransa, zilipungua kwa nusu katika muda wa saa 24, wizara ya mambo ya ndani ilisema, huku watu 72 wakikamatwa kwa usiku mmoja, kote nchini, na kufanya jumla ya watu waliokamtwa kuwa takriban 3,500.