Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:21

Macron alaani ghasia zinazosababisha uharibifu mkubwa Ufaransa


Macron alaani ghasia zinazoendelea Ufaransa
please wait

No media source currently available

0:00 0:04:47 0:00

Macron alaani ghasia zinazoendelea Ufaransa

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa wito kwa wazazi kuwazuia watoto wao kushiriki katika ghasia zinazoendelea kwa usiku wa tatu nchini mwake, huku akisema baadhi ya vijana wanaonekana wakiiga michezo ya video kusababisha ghasia.

Akizungumza baada ya mkutano wa dharura wa kamati ya usalama, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 45 amelaani ghasia hizo akisema kwamba karibu theluthi moja kati ya watu walokamatwa wakati wa ghasia ni vijana au vijana wadogo.

"Zaidi ya shukurani zangu na kuutoa pongezi kutokana na maamuzi tuliochukua, nina maliza hapa kwa kutoa wito kwa wazazi kuwajibika. Ni bayana kwamba kile tunachokishuhudia ni matokeo ya njama iliyopangwa na mara nyingine kuyataka makundi ya watu kuzusha ghasia, jambo ambalo tunalaani, tumewakamata watu, lakini wengi wao ni vijana wadogo. Ni wajibu wa wazazi kuwaweka nyumbani." Amesema rais Macron

Baada ya kikao hicho cha pili cha dharura cha mawaziri siku ya Ijuma, Macron amesema kwamba mitandao ya kijami pia inajukumu kubwa katika kusamba habari za ghasia zilizochochewa na kuuliwa kwa kijana mwenye umri wa miaka 17, Nahel wa asili ya Kitunisia na polisi.

Muandamanaji akibeba bango mjini Montpellier, kusini mwa Ufaranda, linalosema 'Haki itendeke kwa ajili ya Nahel".
Muandamanaji akibeba bango mjini Montpellier, kusini mwa Ufaranda, linalosema 'Haki itendeke kwa ajili ya Nahel".


"Majukwa kwenye mitandao na mitandao ya kijami yanajukumu kubwa katika harakati za siku hizi chache. Tumeona kwenye baadhi yao ikiwa ni Snapchat, Tiktok na nyenginezo, mikusanyiko ya watu ikipangwa na vile vile aina fulani ya ghasia zinazoigizwa kutoka video. Idara za serikali zitakutana na wamiliki majukwa haya ili kutafuta shuluhisho linalostahiki." Amesema rais Macron

Kulingana na wizara ya mambo ya ndani karibu maafisa polisi elfu 40 na wale wa kikosi maalum wamepelekwa katika sehemu mbali mbali za nchi ili kukabiliana na ghasia zinazoongezeka.

Vikosi vya usalama vimeshindwa kuzuia kutiwa moto karibu magari elfu mbili na majengo 492 hasa za serikali na shule na vitu vingine kutiwa moto katika maeneo 3 880 wakati wa siku tatu za ghasia.

Kulingana na takwimu za mwisho za wizara ya mambo ya ndani, watu 875 wamekamatwa wakati wa usiku huku maafisa polisi 249 wamejeruhiwa.

Waandamanaji wakipambana na polisi wa kupambana na ghasia CRS mjini Marseille, kusini mwa Ufaransa hapo June 30, 2023, kufuatia kuuliwa kwa kijana mwenye asili ya Kiafrika na polisi mjini Paris June 27.
Waandamanaji wakipambana na polisi wa kupambana na ghasia CRS mjini Marseille, kusini mwa Ufaransa hapo June 30, 2023, kufuatia kuuliwa kwa kijana mwenye asili ya Kiafrika na polisi mjini Paris June 27.

Usiku wa Ijuma polisi wanaripoti kutokea wizi wa ngawira katika maduka mjini Paris.

Ghasia zimefufua tena hisia na malalamiko ya muda mrefu juu ya jinsi polisi wanavyofanya kazi, hasa kwa kuwabagua wageni wanaoishi kwenye vitongoji vya wakazi wengi kutoka nchi za nje wenye mapato ya chini.

Waziri mkuu wa ufaransa Elizabeth Borne akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu ghasia siku ya Ijuma alisema serikali yake inatafakari kila aina ya suluhisho ili kuzuia kuenea kwa ghasia hizo.

“Kwa hakika ni watu wenye hasira wanaozusha ghasia , na hasa ni vijana wadogo wanaoshambulia vituo vyetu vya polisi, ofisi za meya na majengo ya serikali. Ninataka kusisitiza kwamba watu hawa hawawakilishi wakazi wa miji yewtu ambao wameshtushwa na ghasia hizi.” Amesema Bi. Borne

Wakizungumza kuhusu ghasia hizi wakazi wa kitongoji cha Aubervilliers, baada ya mabasi kumi na tatu kutiwa moto katika kituo kikuu cha basi wanasema, hii inatokana na matatizo ya muda mrefu.

Hadidja Assoumani akizungumza na shirika la habari la AFP anasema kila mara kukitokea tukio na polisi hakuna habari za kweli zinazopatikana.

“Lakini unafikiri kwa nini wamefika katika hali kama hii? Kwangu mimi ni kwa sababu hawana tena matumaini, kwangu mimi ni kwa sababu wanahisi hakuna haki sawa kwa wote, kuna mfumo wa haki kwa aina fulani ya watu na kuna sheria kwa aina nyingine ya watu hilo si jambo zuri.” Amesema Bi. Assoumani

Matukio hayo yote yamesababisha Umoja wa Mataifa kueleza wasi wasi wake kuhusu ubaguzi wa rangi unaofanyawa na polisi wa Ufaransa na kutaka uchunguzi wa kina kufanyika.

Siku ya nne ya ghasia Ufaransa kufuatia kuuliwa kwa kijana na polisi katika kitongoji cha Paris.
Siku ya nne ya ghasia Ufaransa kufuatia kuuliwa kwa kijana na polisi katika kitongoji cha Paris.


Msemaji wa Kamisheni ya Haki za Binadam ya Umoja wa Mataifa amesema huu ni wakati kwa Ufaransa kuchukua hatua za dhati kutanzua tatizo sugu la ubaguzi na sheria za ubaguzi nchini humo.

Forum

XS
SM
MD
LG