Maandamano Misri yaendelea

Gari likiwaka moto katika maandamano ya mjini Giza huko Misri Januari 29 2011.

Kiza kimeingia katika siku ya tano ya maandamano nchini Misri, huku maelfu ya waandamanaji wakikaidi amri ya kutotoka nje na kuendelea na madai yao ya kutaka Rais Hosni Mubarak ajiuzulu.

Serikali ilitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa 10 jioni lakini makundi ya watu yaliendelea kubaki mitaani mjini Cairo na katika miji mingine mikubwa nchini humo.

Jumamosi jioni, Rais Hosni Mubaraka alimteuwa mkuu wa Idara ya Ujasusi nchini humo Omar Suleiman kuwa makamu rais, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mubarak kuteuwa mtu kushika nafasi hiyo. Pia alimteuwa Waziri wa Usafiri wa Anga Ahmed Shafiq kuwa waziri mkuu na kumtaka aunde baraza jipya la mawaziri,

Jumamosi ilikuwa siku ya tano mfululizo ya maandamano ya upinzani yanayotaka kumalizika kwa utawala wa miaka 30 wa Rais Mubarak. Maelfu ya watu walijiunga na maandamano katika miji ya Cairo, Alexandria na Suez.

Mashahidi wameripoti kusikia milio ya bunduki Cairo Jumamosi usiku, na pia kulikuwa na ripoti za uporaji wa mali katika sehemu kadha.