Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, maafisa hao waliotwikwa jukumu la kuendesha mabwawa nchini wamepewa vifungo vya kati ya miaka 9 hadi 27 gerezani, na mahakama ya rufaa ya Derna, wakati wanne miongoni mwao wakiachiliwa huru.
Derna, mji wa pwani wenye wakazi takriban 125,000, Septemba mwaka jana ulikumbwa na mafuriko mabaya yaliosababishwa na kimbunga Daniel. Maelfu ya wakazi walikufa baada ya mabwawa kuvunja kingo, huku wengine wengi wakitoweka. Mkuu huyo wa sheria kwenye serikali ya Tripoli amesema kuwa maafisa watatu miongoni mwa walioshitakiwa wameamurishwa kurejesha fedha walizopata kwa njia ya udanganyifu, kutokana na mkasa huo.
Ripoti ya Januari mwaka huu kutoka Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na EU, ilisema kuwa mkasa huo ulisababisha janga la kimazingira linalohitaji dola bilioni 1.8 za kimarekani, kukarabati. Ripoti hiyo iliongeza kusema kwa kiasi fulani, mabwawa hayo yaliporomoka kutokana na udhaifu wa kiufundi, usimamizi mbaya, pamoja na matatizo ya kiutawala kufuatia ghasia za muda mrefu.