Huku shinikizo likiongezeka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambayo inapaswa kutangaza matokeo ifikapo August 16, maafisa wamefanyakazi usiku kucha kuhesabu kura na kuepusha hofu ya wizi wa kura, huku waangalizi wa uchaguzi wakifuatilia.
“Tunawasihi Wakenya wawe wastahmilivu wakati tunaendelea na zoezi hili kwa makini na tukijitahidi kulikamilisha haraka iwezekanavyo,” Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema katika maelezo aliyoyatoa usiku.
Kufikia saa 10:00am (0700GMT) Jumatano, Kituo cha kujumuisha kura kilikuwa kimepokea takriban asilimia 95 ya fomu za matokeo ya uchaguzi wa urais zilizotumwa kutoka maelfu ya vituo vya kupiga kura.
Wagombea wakuu wa urais, Naibu Rais William Ruto na kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga, wako katika ushindani mkali, matokeo yaliyojumuishwa na vyombo vya habari vya Kenya yalionyesha hivyo. Mgombea atakayeshinda anatakiwa lazima apate asilimia 50% ya kura na kuongeza kura moja.
Lakini wasomi wanaofuatilia majumuisho ya vyombo vya habari walisema wamegundua kuna dosari fulani, na kutahadharisha kuwa matokeo hayo siyo rasmi.
Iwapo wote Ruto au Odinga hawatapata zaidi ya asilimia 50 ya kura, Kenya italazimika kupiga kura raundi ya pili kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.
Tume ya Uchaguzi, IEBC, ilichapisha picha za zaidi ya asilimia 95 ya fomu za matokeo ya uchaguzi, kutoka jumla ya vituo vya uchaguzi 46,663.
Tume hiyo inachapisha picha, na siyo takwimu. Ni matokeo mawili kati ya matokeo 290 ya majimbo ya uchaguzi yamewekwa katika tovuti ya tume hiyo.
Fomu za Matokeo katika jimbo ni lazima zilinganishwe katika kituo cha kupiga kura na kupelekwa hadi kituo cha kitaifa cha kujumuisha cha mji mkuu, Nairobi, na ithibitishwe kabla ya tume kutoa matokeo rasmi.
Mchakato huo ni kutokana na maamuzi ya Mahakama ya Juu ya 2017 iliyokataa matokeo ya awali ya kuchaguliwa tena Kenyatta mwezi Agosti katika mwaka huo, ikieleza kushindwa kwa tume kufuata machakato huo kisheria.
Matokeo ya mwisho kutoka IEBC yanatarajiwa kuchukua siku kadhaa, japokuwa kisheria, ina muda wa wiki moja kutoa matokeo hayo.
Idadi ya waliojitokeza kupiga kura Jumanne Kenya ilikuwa chini, wakati wapiga kura pia walichagua wabunge na wawakilishi wa maeneo.
Upigaji kura Jumanne kwa kiasi kikubwa ulikuwa wa amani, japokuwa polisi walisema walikuwa wanamtafuta mwakilishi aliyempiga risasi msaidizi wa mpinzani wake nje ya kituo cha kupiga kura. Katika mji wa kaskazini wa Eldas, ambapo ghasia zilizuia uchaguzi usifanyike Jumanne, vituo vya kupiga kura vilifunguliwa kwa amani Jumatano, maafisa wa uchaguzi walisema.
Kulingana na takwimu za karibuni za IEBC, waliojitokeza Jumanne saa saa kumi alasiri baada ya upigaji kura kuanza, ilikuwa ni asilimia 56 ya wapiga kura milioni 22 waliojiandikisha.
Hiyo ikilinganishwa na idadi kamili ya mahudhurio ya wapiga kura ya asilimia 78 katika uchaguzi uliokuwa na utata wa Agosti 2017.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP