Kundi la kwanza la watu waliojeruhiwa Gaza lavuka mpaka kuingia Misri

Waandishi wa habari wakichukua picha za video wakati magari ya wagonjwa ya wizara ya afya ya Palestina yakivuka lango kuingia katika kivuko cha Rafah upande wa kusini mwa Ukanda wa Gaza kabla ya kuingia Misri Novemba 1, 2023.

Kundi la kwanza la watu waliojeruhiwa kutoka  Gaza limevuka  mpaka kuingia Misri Jumanne chini ya makubaliano ya mpango uliosimamiwa na Qatar, vyombo vya habari vya Misri na chanzo cha habari kwenye eneo la mpaka wamesema.

Wakati huo huo vikosi vya Israel vimekuwa vikiongeza mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika maeneo ya Palestina.

Watu waliondolewa walisafirishwa kwa magari ya kubeba wagonjwa kupitia kivuko cha mpakani cha Rafah.

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya Misri, Israel, na Hamas, idadi ya raia wa kigeni na watu waliojeruhiwa vibaya wataruhusiwa kuondoka katika eneo lililozingirwa.

Kuondolewa huko kwa watu kunafuatia siku nyingine ya umwagaji damu huko Gaza ambako mashambulizi ya anga ya Israel Jumanne yaliuwa watu 50 katika kambi ya wakimbizi kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Palestina.

Kulingana na Israel shambulizi hilo limemuuwa kamanda wa Hamas na wapiganaji wengine wengi.

Taarifa iliyotolewa na vikosi vya usalama vya Israel baadaye walimtambua mwanaume mmoja kama Ibrahim Biari na kusema alikuwa kiongozi wa mauaji ya kigaidi ya octoba 7 yaliyofanywa na wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel.

Israel ilituma wanajehi wake GAZA inayodhibitiwa na Hamas kufuatia wiki za mashambulizi ya anga na ya makombora ikiwa ni kujibu shambulizi lililofanywa na kundi hilo la wanamgambo wa Kiislamu kusini mwa Israel.