Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema Jumamosi kimbunga Jobo kilichokuwa kinatarajiwa kupiga pwani ya Tanzania kwa siku mbili, Jumamosi na Jumapili kimepungua nguvu.
Kupungua nguvu huko kwa haraka kumesababishwa na kimbunga hicho kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani hivyo kwa sasa ni kimbunga hafifu kinachosafiri kwa kasi ya kilometa 18 kwa saa baharini.
Taarifa ya mamlaka imeongeza kuwa kimbunga hicho kwa sasa kipo umbali wa kilometa 200 Mashariki mwa kisiwa cha Mafia na kupungua kwake nguvu kunatarajiwa kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo machache ya ukanda wa Pwani kati ya leo na kesho, huku pia kikisababisha mawimbi makubwa baharini.
Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikiwemo Kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam na kisiwa cha Unguja.