Kenya ilisema kuwa ingetuma polisi 1,000 ili kurejesha udhabiti nchini Haiti kwa ushirikiano na wenzao kutoka mataifa mengine, lakini hatua hiyo imekumbwa na vizingiti vya kisheria. Rais wa Kenya William Ruto amekuwa kwenye mstari wa mbele kuunga mkono mpango huo, wakati akiahidi mapema mwezi huu kwamba ungeanza ndani ya wiki kadhaa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba mwaka jana liliidhinisha kupelekwa kwa kikosi hicho, lakini mahakama moja ya Kenya ikachelewesha hatua hiyo Janurari. Kando na Kenya, mataifa mengine yaliyoelezea nia yao ya kujiunga na kikosi hicho ni pamoja na Benin, Bahamas, Bangladesh, Barbados na Chad.
Marekani inatoa ufadhili, pamoja na msaada wa kiufundi, bila kutuma wanajeshi wake moja kwa moja kwenye taifa hilo masikini zaidi la Caribbean. Shirika la kimtaifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limeelezea wasi wasi wake kuhusu hatua hiyo wakati pia likihoji ufadhili wake.