Ruto amesema yeye na waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry walijadili hatua zinazofuata kwa ajili ya kuwezesha upelekaji wa haraka, lakini haikuwa wazi mara moja kama makubaliano hayo yataingilia maamuzi ya mahakama yaliyotolewa mwezi Januari yaliyosema kwamba hatua ya kupeleka polisi Haiti ni kinyume cha sheria.
Kenya awali ilisema kwamba ilikuwa tayari kupeleka maafisa wa polisi 1,000 hatua ambayo ilipokelewa vyema na Marekani na mataifa mengine ambayo yalifuta uwezekano wa kupeleka vikosi vyake huko.
Lakini mahakama ya Nairobi ilisema kuwa uamuzi huo ulikuwa kinyume cha katiba kwa sehemu kwa sababu nchi hizo hazijatia saini makubaliano ya pande mbili kuhusiana na suala hilo.
Leo Ruto amesema yeye na Henry wameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya pande mbili katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kupelekwa ujumbe huo mwezi Oktoba mwaka jana lakini wasiwasi nchini Kenya kuhusu polisi hao kuhusika ulipelekea maamuzi hayo ya mahakama.