Kenya kuendeleza juhudi za kutokomeza ugonjwa Ukimwi

jiji la Nairobi, Kenya

Serikali ya Marekani imetangaza kuwa itaendelea kuwa sehemu ya juhudi za ushirikiano katika kutokomeza kabisa ujonjwa wa UKIMWI.

Kupitia balozi wake jijini Nairobi, Meg Whitman, serikali ya Marekani imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Kenya ili kudhibiti kabisa janga hilo na kulitokomeza tishio la VVU/UKIMWI kama afya ya umma.

Katika maadhimisho ya miaka 20 ya Mpango huo wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi unaojuliakana kama PEPFAR, rais William Ruto ameishukuru serikali ya Marekani na kueleza kuwa Kenya imepiga hatua za wazi na muhimu ambazo zimebadilisha hali ya taifa la Kenya kwa kuziwezesha jamii nyingi kujilinda dhidi ya makali ya virusi vya ukimwi.

Ruto anaeleza kuwa ushirikiano huu kupitia PEPFAR, umesababisha mabadiliko ya moja kwa moja, ya binafsi, yanayoonekana katika maisha na ustawi wa raia wa Kenya katika juhudi za kukomesha mateso, kupunguza idadi ya vifo na kurefusha maisha ya mamilioni ya wananchi wa Kenya ambao wamekuwa wakikabiliwa na hatari kubwa ya kifo na makovu ya kudumu yanayosababishwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Madawa kwa ajili ya wagonjwa wenye Upungufu wa kinga Mwilini (UKIMWI)

Kupitia mpango huo, serikali ya Marekani imeipatia Kenya zaidi ya dola bilioni 6.5 za Kimarekani tangu mwaka 2004. Mwaka wa Fedha wa 2023/4, Marekani imeipa Kenya mgao wa dola milioni 346.2 huku mwaka ujao wa kifedha 2024/5 Kenya itapokea mgao wa dola milioni 327.9.

Rais Ruto anasema kuwa msaada huo wa kupitia PEPFAR, Kenya imeweza kupunguza kwa asilimia 68.5 maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na vile vile kupunguza asilimia 53 ya vifo vinavyosababishwa na virusi hivyo.

Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini Kenya ni milioni 1.4. Watu milioni 1.3 kati ya hawa wanaendelea kupata tiba na dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi kwenye vituo vya afya 3,000 kote nchini Kenya.

Tatizo la virusi vya ukimwi linaigharimu Kenya kati ya shilingi bilioni 27 kadi 30 kila mwaka kutokana na kupungua kwa ufadhili, pengo lililopo la ufadhili ni dola milioni 11.7 za Kimarekani.

Ili kukabiliana na pengo hilo la ufadhili, rais Ruto amesema serikali yake imedhamiria kuongeza ufadhili wa ndani hatua kwa hatua kuendeleza mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika ubia na serikali ya Marekani kupitia mpango huyo wa PEPFAR.

Kenya inalenga kuutokomeza ugonjwa wa ukimwi kwa watoto ifikapo 2027.

Naye Christina Makumi, kutoka shirika la kimataifa la jamii ya wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini Kenya, ICW anaeleza kuwa mpango wa PEPFAR umeleta mafanikio makubwa nchini Kenya na juhudi hizo zinastahili kuongezwa na serikali.

Shirika la kupambana na ugonjwa wa ukimwi la Umoja wa Mataifa, UNAIDS, shirika la Afya Duniani WHO na shirika la Idadi ya watu la umoja huo, UNFPA kwa ushirikiano na serikali ya Kenya na mashirika mengine miezi michache iliyopita zimetangaza Hati fungani za Maendeleo ya Matokeo ya Muda Mrefu kama juhudi shirikishi za kukuza huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana ili kuimarisha upimaji na matibabu ya VVU miongoni mwa vijana hasa kwa wasichana waliobalehe wenye umri wa kati ya miaka 15-19.

Mashirika hayo yametoa ufadhili wa dola milioni 10.1 za Kimarekani kuwezesha nguvu za umma na za kibinafsi kukomesha tatizo la mimba za utotoni na maambukizi mapya ya VVU na kuwezesha upatikanaji wa huduma rafiki za afya ya uzazi kuondoa vifo vinavyotokana na ukimwi miongoni mwa wasichana walio katika mazingira magumu nchini Kenya, kwa kulenga changamoto kama vile ukosefu wa taarifa kuhusu afya ya uzazi, upatikanaji duni wa huduma zinazowalenga vijana na wale wanaopitia manyanyaso ya kingono.

Nchini Kenya, wasichana waliobalehe na watoto wakike wako hatarini zaidi, kwani data zinaonyesha kuwa asilimia 78% ya maambukizo mapya ya VVU ni yanatoka kwenye kundi hilo.

Kenya inalenga kukomesha VVU na UKIMWI kama tishio kwa afya ya umma na mimba za utotoni kufikia mwaka 2030 na ukatili wa kijinsia ifikapo 2026.

KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.