Kashfa ya Deni la Msumbiji : Marekani yataka Chang awajibishwe

Manuel Chang

Serikali ya Marekani inataka waziri wa zamani wa fedha wa Msumbiji, Manuel Chang, kuwajibishwa kwa jukumu lake katika kashfa ya deni lenye thamani ya dola bilioni 2, ambalo limelitumbukiza taifa hilo la kusini mashariki mwa Afrika katika mzozo mkubwa wa kifedha.

Msumbiji inamtaka waziri huyo anayeshikiliwa Afrika Kusini kurudishwa nyumbani.

Waziri Chang alikamatwa Johanesburg akielekea Dubai na ripoti ya mwandishi wetu huko Afrika Kusini, Anita Powell, inaeleza kwamba mahakama moja ilisikiliza kesi yake na mawakili wa Msumbiji na Marekani walitowa hoja zao kuthibitisha nchi gani anahitajika zaidi.

Kesi inayohusisha mabara manne

Marekani inamtaka kwa kuhusika katika kesi kubwa ya ubadhirifu wa mali unaohusisha mabara manne, Afrika, Amerika ya Kaskazini, Ulaya na Asia. Chang ni moja wapo wa darzeni za watu walohusishwa katika pande zote za Bahari ya Atlantic.

Mashtaka yaliyofunguliwa katika mahakama ya wilaya ya mashariki ya New York yanamtuhumu Chang na watu kadhaa baadhi ambao hawajatajwa bado kwa kubuni mradi wa usafiri wa baharini kama jukwa la kukusanya fedha ili kujitajirisha na kwa makusudi kuchukuwa sehemu ya mkopo kujilipa kwa njia ya hongo karibu dola milioni 200, pamoja na maafisa wa serikali ya msumbiji na watu wengine.

Baada ya ombi la Marekani

Na mara tu baada ya ombi la Marekani kufika katika mahakama ya Afrika Kusini kumtaka akabidhiwe Marekani, msumbiji iliwasilisha ombi kupinga jambo hilo na kumtaka arudishwe nyumbani. Lakini kufuatana na maafisa wa Afrika Kusini, Maputo haijatowa hati ya kukamatwa kwake kwa hivyo haifahamiki kwa nini wanamtaka.

Mkopo huo wa siri ulisababisha taifa hilo linalopakana na Bahari ya Hindi kukabiliwa na shida kubwa ya deni hata kupelekea wananchi wake kukosa baadhi ya huduma muhimu za umaa.

Huduma hizo zinajumuisha kukarabati barabara na kuendesha hospitali za serikali. Serikali imeshawakamata karibu watu 18 kuhusiana na kashfa hiyo.

Lakini wakosoaji wa Serikali wanasema wanashaka kama kuna kitu kitakachofanyika kuhusiana na waliyokamatwa au hata kushtakiwa nchini Msumbiji kutokana na kesi hiyo.

Kauli ya Jaji

Jaji wa Afrika Kusini anayesikiliza kesi hiyo, William Schutte, amesema hakuna kinachofahamika juu ya kesi hii. Anasema inaonekana wanajikuta katika tukio la kisheria ambalo halijawahi kutokea.

Schutte hivi sasa anakabiliwa na jukumu kubwa la kuamuwa iwapo Chang asafirisahwe, na ikiwa hivyo ndivyo apelekwe wapi.

Wakili wa Chang, Willie Vermuelen ameeleza bayana kwamba mteja wake angelipendelea arudishwe nyumbani na kumhimiza jaji kutafakari juu ya ombi hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Afrika Kusini aliviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo wiki iliyopita kwamba nchi hiyo itamruhusu arudishwe Msumbiji.

Mwendesha Mashtaka nchini humo, JJ du Toit alikasirishwa na matamshi hayo na kusema kuwa waziri wa sheria ndiye mwenye mamlaka ya juu katika suala hilo.

Chang alikuwepo mahakanani akiwa ametulia wakati wakili wakibishana. Waziri huyo wa zamani aliyekuwa anaelekea katika sherehe ya kifamilia Dubai kupitia Afrika Kusini hivi sasa anarudishwa rumande hadi kesi yake itakaposikilizwa tena machi 7.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC.