Kamati ya Upelelezi yaendelea kusikiliza ushahidi unaolenga kumuondoa Trump madarakani

Fiona Hill

Baada ya siku ndefu iliyokuwa na ushahidi mzito mbele ya kamati ya upelelezi katika bunge la Marekani hapo Jumatano kuhusu uchunguzi wa kutaka kumfungulia mashtaka ya kumuondoa madarakani Rais Donald Trump, Alhamisi wabunge watasikiliza ushahidi wa Fiona Hill.

Hill aliyewahi kuwa mtaalam wa Russia kwenye Baraza la Usalama wa Taifa ambaye awali aliwaeleza wana kamati katika kikao cha faragha kwamba aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Ukraine aliondolewa kutokana na kampeni ilioanzishwa na wakili wa Trump.

Mwingine atakayetoa ushahidi ni David Holmes ambaye ni mtaalam wa maswala ya mambo ya nje ambaye anahudumu katika ubalozi wa Marekani mjini Kyiv, Ukraine.

Holmes alisema katika kamati hiyo ya upelelezi kuwa alisikia simu ya Trump kwa balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Ulaya, Gordon Sondland, akimuuliza iwapo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, angeanzisha uchunguzi dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden.

Lakini Trump amekuwa akikanusha kuzuia msaada wa karibu dola za Marekani milioni 400 kwa Ukraine, hadi pale watakapo tangaza kufanya uchunguzi dhidi ya Biden.