Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, taarifa kutoka kwa naibu kamanda wa jeshi Yasser al- Atta, imesema kwamba jeshi limepiga hatua mjini Omdurman ambayo ni sehemu ya mji mkuu wa Khartoum, wakati kukiwa na wito kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa ajili ya sitisho la mapigano katika mwezi huu mtukufu wa Ramadan ambao unaonza wiki hii.
Kundi la kijeshi la Rapid Support Forces, RSF, kwa upande wake limesema kuwa linakaribisha wito wa kuwa na sitisho la mapigano. RSF limesema Jumapili kwamba jeshi limekataa ombi lake la kuachiliwa kwa wafungwa wa vita 537, wanaoshikiliwa, kupitia kamati ya Kimataifa ya Mslaba Mwekundu.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ametoa wito wa sitisho la mapigano wakati huu wa Ramadhan. Balozi wa Sudan kwenye UN Alhamisi aliliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba kiongozi wa jeshi na mkuu wa Baraza la uongozi Abdel Fattah al Burhan, walipongeza wito wa Guterres, lakini walikuwa wakitafakari namna utakavyotekelezwa.