Jeshi la Sudan lafanya mashambulizi ya mizinga na ya anga Khartoum

Shambulizi lililofanywa na Jeshi la Sudan mjini Khartoum Septemba 26, 2024.

Jeshi la Sudan limefanya mashambulizi ya mizinga na ya anga  katika mji mkuu wa Sudan Alhamisi  katika operesheni kubwa sana  ya kukomboa tena maeneo ya huko tangu vita vyake vya miezi 17 kuzuka na   vikosi vya RSF , mashahidi na vyanzo vya  jeshi vimesema.

Msukumo wa jeshi ambalo lilipoteza udhibiti wa eneo lote la mji mkuu mwanzoni mwa mzozo , umekuja kabla ya rais wa sudan Abdel Fattah al Burhan kuhutubia baraza kuu la umoja wa mataifa baadae leo mjini New York.

Mashahidi wameripoti mashambulizi mazito ya mabomu na mapigano baina ya vikosi vya jeshi vikijaribu kuvuka madaraja katika mto nile unaounganisha miji mitatu Khartoum, Omdurman na Bahri inayounda mji mkuu.

Ingawa jeshi ilichukua tena baadhi ya eno katika mji wa Omdurman mapema mwaka huu , linategemea zaidi silaha na mashambulizi ya anga na halijaweza kuviondoa vikosi vya RSF vilivyopo katika maeneo mengine ya mji mkuu.

Hata hivyo RSF nayo inaendelea kusonga mbele katika baadhi ya maeneo mengine Sudan katika miezi ya karibuni kwenye mzozo ambao umesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu na kukosesha makazi watu milioni 10 na kupelekea maeneo mengine ya nchi kuwa na njaa kubwa na ukame.