Jenerali al-Burhan wa Sudan kuhutubia Baraza Kuu la UN

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alipo hutubia kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York City, Septemba 22 2022. Picha na REUTERS/Mike Segar

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye yuko vitani kwa miezi kadhaa na wanamgambo, ameelekea New York siku ya Jumatano kuhutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ofisi yake imesema.

Burhan, kiongozi mkuu wa Sudan tangu mapinduzi ya mwaka 2021, "ataongoza ujumbe wa Sudan" kwenye kikao cha mwaka, Baraza la Uhuru analoliongoza limesema katika taarifa yake.

Mkuu wa jeshi amekuwa akifanya mfululizo wa ziara nje ya nchi katika wiki za hivi karibuni baada ya kuhamisha kambi yake kwenda Port Sudan mwishoni mwa mwezi uliopita kutoka makao makuu ya jeshi mjini Khartoum ambako alikuwa amezingirwa na wanajeshi wa kikosi cha RSF cha naibu wake wa zamani Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, tangu mapigano yalipozuka Aprili 15.

Wachambuzi wamesema mpango wake wa kidiplomasia ni kufanya harakati za kuutafuta uhalali wake endapo kutakuwa na mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Burhan tayari ametembelea nchi za Misri, Sudan Kusini, Qatar, Eritrea, Uturuki na Uganda.

Katika ziara yake ya Umoja wa Mataifa, Burhan anakusudia kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na atahudhuria "mikutano ya ngazi ya juu" pembeni ya mkutano mkuu, ilisema taarifa hiyo.

Mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya takriban watu 7,500, kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la Acled na Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni tano wamekimbia makazi yao.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP