Picha hizo za video zilipigwa na vyombo vya usalama vya Uturuki na kuonyeshwa Jumatatu na CNN, zikiwa zinaelekeza kuwa jasusi wa Saudia alijifananisha na mwandishi huyo ikiwa ni juhudi ya kuweza kuficha mauaji hayo.
Video hiyo ilitolewa wakati maafisa wa Saudia walikuwa kwa mara nyingine tena wanatoa maelezo juu ya kifo cha mwandishi wa Saudia mwenye umri wa miaka 59 ambaye alikuwa anaishi Marekani, ambako aliamua yeye mwenye kuwa mkimbizi wakati akiendelea kuandika Makala kwenye gazeti la The Washington Post ambazo zilikuwa zinamkosoa vikali Prince Mohammed bin Salman na Riyadh kwa kujihusisha na vita ya Yemen.
Hapo awali Saudia ilikuwa inasema Khashoggi aliondoka ubalozini na hawajui alikokuwa amekwenda.
Baadae, walisema kuwa alikufa wakati wa akirushiana ngumi baada ya mzozo kutokea ndani ya ubalozi. Saudia hivi sasa inasema kuwa Khashoggi alikufa baada ya kupigwa kabari ikiwa ni hatua ya kumzuia asiondoke ubalozini wakati akijaribu kutoka nje kutafuta msaada.
Hata hivyo haijulikani mwili wa Khashoggi ulifanywa nini, japokuwa maafisa wa Uturuki wanasema alikuwa ameteswa, na kukatwa kichwa na mwili kukatwa vipande vipande.
Afisa mmoja wa Saudia ameiambia shirika la habari la ABC kuwa mwili wa Khashoggi ulikabidhiwa kwa “msaidizi ndani ya nchi” mjini Istanbul kuutupa, lakini maafisa wa Saudia wamesema hawajui mwili wake ulichofanyiwa.
Mjini Washington, mshauri wa White House Jared Kushner, mkwe wa Rais Donald Trump, ameliambia shirika la habari la CNN kuwa Marekani bado iko katika hatua ya “kufanya uchunguzi” ili kufahamu nini hasa kilicho mtokea Khashoggi.
“Tunajaribu kukusanya ushahidi kutoka sehemu mbalimbali,” Kushner amesema. Amesema kuwa Trump na Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo hapo baadae wataamuwa jinsi ya kuwajibu Saudi Arabia, mshirika wa muda mrefu wa Marekani.
Saudi Arabia imesema Mohammed amezungumza Jumatatu kwa simu na mtoto wa kiume wa Khashoggi akitoa mkono wa pole kwa mauaji ya baba yake.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameahidi kutoa vielelezo zaidi juu ya mauaji hayo wakati atakapotoa hotuba yake Jumanne bungeni.