"Imethibitishwa na upande wa usalama na Wizara ya Mambo ya Nje kwamba mateka 12 wa Thailand tayari wameachiliwa," aliandika kwenye mtandao wa X.
"Maafisa wa Ubalozi wapo njiani kuwachukua katika saa moja ijayo, majina yao na maelezo yao ni vyema yafahamike. Tafadhali endelea kufuatilia."
Jumla ya raia 25 wa Thailand walikuwa miongoni mwa watu wanaokadiriwa 240 waliotekwa nyara na watu wenye silaha wakati wa mashambulizi ya mwezi uliopita yaliyovuka mpaka kuingia Israel.
Israel imelipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi makubwa ya anga, mizinga na jeshi la majini sambamba na mashambulizi ya ardhini katika eneo la Gaza, ambalol inatawaliwa na Hamas.
Serikali ya Hamas inasema vita hivyo vimeua takriban watu 15,000, maelfu kati yao ni watoto.
Siku ya Ijumaa, sitisho la mapigano lilianza baada ya wiki kadhaa za mazungumzo yaliyosimamiwa na Qatar, Misri na Marekani.
Chini ya makubaliano hayo, sitisho la vita litadumu kwa siku nne na kushuhudia mateka wasiopungua 50 wataachiliwa kutoka Gaza, kwa mabadilishano ya wafungwa 150 wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel.
Vyanzo viwili vya Hamas vililiambia shirika la habari la AFP siku ya Ijumaa kwamba baadhi ya mateka waliokamatwa katika uvamizi huo Ijumaa walikabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu ili kurejeshwa Israel, kupitia Misri.
Muda mfupi baada ya waziri mkuu wa Thailand kuchapisha kwenye X, chanzo karibu na Hamas kiliithibitishia AFP kwamba baadhi ya mateka wa Thailand wameachiliwa, pamoja na ongezeko la mateka walioachiliwa chini ya makubaliano na Israel.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP