Familia kutoa Sh1b/- kwa atakaye fanikisha kupatikana Dewji

Mfanyabiashara mashuhuri wa Tanzania Mohammed Dewji .Aprili 23, 2015.

Familia ya Gulam Dewji imetangaza donge nono la shilingi bilioni 1 kwa yeyote atakaye fanikisha kupatikana kwa mtoto wao mfanyabiashara mashuhuri Mohammed Dewji, maarufu kama Mo.

Mo alitekwa na watu wasiojulikana akiwa katika hotel ya Colosium Oysterbay jijini dar es salam afajiri ya Alhamisi wiki iliyopita alipokuwa ameenda kufanya mazoezi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, msemaji wa familia ya Dewji Azim Dewji ameishukuru serikali kwa juhudi zake za kumtafuta Mo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa makampuni ya Mohammed Enterprises Limited.

Msemaji huyo wa Familia ya Mo ameahidi kwamba atakayetoa taarifa zitabaki kuwa siri baina ya familia na yeye kwani zinalenga kuwezesha kupatikana kwa Mohammed Dewji.

“Katika kuhakikisha mtoto wetu mpendwa anapatika mapema tunatangaza donge nono la Shilingi bilioni 1 kwa yeyote atakayetoa taarifa muhimu zitakazo pelekea kupatikana kwake na taarifa hizo zitakuwa ni siri kati ya mtoa taarifa na familia yetu," alisema Azim.

Kwa yeyote mwenye taarifa anaweza kuwasiliana na familia hiyo kupitia namba za simu 0755 030 014, 0717 208 478 na 0784 783 228.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu na kisha tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi zake kwa jitihada kubwa wanazo zifanya katika kuhakikisha kwamba mtoto wetu anapatikana, vyombo vya habari kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kulichukulia uzito jambo hili na kutoa taarifa kwa Umma, taasisi za kidini na zisizo za kidini na kila mmoja wenu kwa maombi ya kutufariji katika kipindi hiki kigumu familia inachopitia,“ alisema Azim.

Katika hatua nyingine , katika mkutano na waandishi wa habari Jjijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii, Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola amesema jeshi la polisi linaendelea kuchunguza na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha linampata mfanyabiashara Mohamed Dewji aliyetekwa Alhamis iliyopita Asubuhi wakati akienda mazoezi katika gym ya Collasseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Aidha Waziri Lugola amesema mpaka sasa jeshi la Polisi limewatia mbaroni watu zaidi ya ishirini katika sakata hilo la kutekwa kwa Mo ambao wanaendelea kuhojiwa na Polisi.

Aidha waziri Lugola pia amewataka wananchi kuendelea kuliamini jeshi la Polisi na vyombo vyote vya dola na kuwahakikishia wananchi kuwa pamoja na kuibuka kwa tukio hilo hali ya usalama nchini imeimarika lakini pia serikali itaendelea kupambana na matukio yote ya uhalifu.

Hata hivyo waziri Lugola amevitaka vyombo vya habari hususan mitandao ya kijamii kuwa makini katika utoaji wa taarifa kutokana na utoaji taarifa za kuwakanganya wananchi zikiwemo za kupotosha dhidi ya tukio hilo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Dinnah Chahali, Tanzania.