Dazeni ya watu waendelea kutafutwa kufuatia maporomoko Ufilipino

Waokoaji wakiwatafuta watu waliokuwa wamefunikwa ndani ya maporomoko ya ardhi yaliyo sababishwa na kimbunga Mangkhut katika kambi inayo fanya machimbo madogo huko kitongoji cha Itogon, Benguet, Ufilipino, Septemba 17, 2018.

Meya wa mji mdogo Ufilipino amesema “anauhakika kwa asilimia 99” kuwa dazeni za watu waliokuwa hawajapatikana katika maporomoko ya ardhi yaliyo sababishwa na Kimbunga Mangkhut wameuwawa.

Miili kumi na moja imeshatolewa kutoka katika kifusi katika mji wa Itogon upande wa ncha ya kaskazini ya kisiwa kikuu cha Luzon, ambacho kilipata dharuba kali wakati kimbunga Mangkhut kilipowasili Jumamosi kikiwa na upepo mkali unaokwenda kilomita 270 kwa saa. Kupatikana kwa miili hiyo 11 imefanya idadi ya waliokufa Ufilipino kufikia 65 kutoka ile ya 54.

Mayor wa Itogon Victorio Palangdan amesema wahanga walikuwa ni wachimbaji wa madini na familia zao ambazo zilikuwa zimehamia katika nyumba ya ardhini ya zamani katika machimbo hayo, wakijikinga na kimbunga hicho, ambayo ilikuwa imegeuzwa kuwa kanisa. Watu wasio pungua 40 inaaminika kuwa ni katika wale waliokuwa hawajulikani waliko na wengine wanaodhaniwa kuwa wamekufa.

Maafisa wanao shughulikia matukio ya dharura hawakuweza kuleta vifaa vikubwa vya uokoaji katika eneo la Itogon kutokana na maporomoko hayo kuacha njia kuwa hazipitiki, ikiwalazimu waokoaji hao kuchimba kifusi kwa kutumia makoleo na mikono yao.

Itogon iko katika mkoa wa Cordillera, ambako maafisa wametahadharisha kuwa shughuli za uchimbaji zinazo endeshwa kisheria au kinyume cha sheria katika eneo hilo zimesababisha pande za milima hiyo kuwa ni hatarishi kunapokuwa na maporomoko.

Waziri wa Mazingira Roy Cimatu Jumatatu ameagiza kusitishwa mara moja shughuli za uchimbaji katika eneo la Cordillera.

Mashamba eneo lote la Luzon, kisiwa kikubwa kuliko vyote Ufilipino, yamefunikwa na mafuriko. Mashamba ya Luzon yanazalisha sehemu kubwa ya mpunga na mahindi yanayo limwa nchini humo. Na hivi sasa mazao yao yameharibiwa kabisa, ikiwa tu imebakia mwezi mmoja kuvuna.