Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, taarifa hiyo ya Jumanne, ni kutoka kwa vyanzo 6 vyenye ufahamu wa kina wa suala hilo. Hatua hiyo itapunguza jukumu la makampuni makubwa ya kimataifa ya mafuta, ambayo kwa miezi kadhaa yamekuwa yakishauriana kuhusu kupeleka mafuta ghafi kwenye kiwanda hicho, pamoja na ufadhili wa kifedha, kwa mabadilishano ya bidhaa za mafuta.
Kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 650,000 kwa siku, kinatarajiwa kutikisa soko la kimataifa la mafuta. Dangote ambaye utajiri wake umeripotiwa kuwa wenye thamani ya takriban dola bilioni 12.7 za kimarekani kulingana na jarida la Forbes, bado hajajibu chochote kuhusu maombi kadhaa yanayomtaka atoe maoni yake.
Makampuni ya mafuta ya BP, Trafigura na Vitol, ni miongoni mwa kadhaa ambayo yamefanya vikao na Dangote mjini Lagosna London katika wiki za karibuni, yakionyesha ari ya kutoa mkopo wa dola bilioni 3 zinazohitajika kuendesha kiwanda hicho.