COVID-19 : Magufuli asema serikali haitaweka masharti ya biashara

Gari lililobeba mwili wa Katibu Kiongozi wa Tanzania marehemu John Kijazi.

Rais wa Tanzania, John Magufuli, amesema serikali yake haitaweka masharti ya kusitisha shughuli za kibiashara, katika kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.

Magufuli amesema hayo wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi, katika uwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Kwa mara nyingine tena, rais huyo amewataka Watanzania kumtegemea Mungu, na kuongeza kuwa Tanzania ilishinda mwaka jana, mpaka ikaingia uchumi wa kati, huku ugonjwa wa Corona ukiwepo.

Amewaambia waliohudhuria ibada hiyo kwamba, mwaka 2020, utawala wake haukuweka masharti makali ya kusitisha shughuli za biashara, na kwamba hata sasa, hautafanya hivyo.

Kauli yake imejiri siku moja baada ya mazishi ya aliyekuwa makamu war ais wa kwanza wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad aliyefariki siku ya Jumatano, baada ya kuugua ugonjwa wa Covid-19.

Kumekuwa na tetesi kwamba visa vya maambukizi ya Corona nchini humo, vinazidi kuongezeka, licha ya kwamba hakuna takwimu rasmi zilizotolewa na serikali tangu mwezi Mei mwaka 2020.