Blinken afanya ziara ya siku mbili Ukraine huku Russia ikiendelea na mashambulizi ya angani Kyiv

Picha hii imetolewa na wizara ya mambo ya nje ya Ukraine inamuonyesha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani , Antony Blinken, kulia, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, wakizuru makaburi ya mashujaa huko Berkovetske in Kyiv, Sept. 6, 2023, in Kyiv, Ukraine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken yuko Kyiv kwa ziara ya siku mbili ya kushitukiza, ikiwa ni ya nne nchini  Ukraine tangu Russia kuivamia nchi hiyo mwezi Februari 2022.

Blinken amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, Waziri Mkuu Denys Shmyhal na Rais Volodymyr Zelenskyy kusikiliza tathmini yao ya mahitaji yote kwa ajili ya kujibu mashambulizi dhidi ya Russia na pia majira ya baridi yanayokaribia.

“Tumeona maendeleo mazuri katika kujibu mashambulizi.

Tunataka kuhakikisha kuwa Ukraine inacho kile inachohitaji siyo tu kufanikiwa katika kujibu mashambulizi lakini inacho kile inachohitaji kwa ajili ya muda mrefu kuhakikisha kuwa inakizuizi imara, uwezo imara wa kujilinda ili, siku za usoni, uchokozi kama huu usijirejee tena,” Blinken alisema kabla ya mazungumzo yake na viongozi hao Jumatano.

Kuna uwezekano Blinken atatangaza msaada mpya wa Marekani wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 1, afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje aliwaambia waandishi wakati wakiwa safarini.

Saa kadhaa kabla ya kuwasili, Russia ilifanya mashambulizi ya anga mjini Kyiv na mkoa wa kusini wa mji wa Odesa. Hakuna vifo vilivyo ripotiwa katika mji mkuu huo, lakini maafisa wa Ukraine walisema raia mmoja aliuawa na miundombinu ya bandari iliharibiwa upande wa kusini.

Wizara ya Mambo ya Nje inasema Blinken anakusudia kuonyesha uungaji mkono imara wa Marekani kwa Ukraine, na kuratibu pamoja na viongozi huko Ukraine kabla ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) huko New York wiki ijayo, ambapo Washington itaongoza kushinikiza Kyiv kuendelea kuungwa mkono.

Mwisho…