Biden, Sanders wako tayari kupambana uchaguzi wa 'Super Tuesday'

Seneta Bernie Sanders na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden, aliyeshinda kwa urahisi uchaguzi wa awali uliofanyika South Carolina, anakabiliwa hivi sasa na changamoto mpya kutoka kwa Seneta wa Vermont Bernie Sanders wakati majimbo 14 watakapopiga kura Jumanne katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa chama.

Biden, katika uchaguzi wa majimbo matatu akiwania nafasi ya urais, alikuwa hajashinda hata mara moja hadi Jumamosi. Lakini utafiti kabla ya uchaguzi unaonyesha kuwa Sanders, mdemokrati mwenye msimamo wake wa mrengo wa kushoto wa kisoshalisti anaonekana kuongoza katika jimbo la California.

Katika kinyang'anyiro hicho wajumbe wa mkutano wa kitaifa wa kumteua mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho utakaofanyika katika kipindi cha joto watakuwa na jukumu muhimu katika kumteua mgombea kukiwakilisha chama wakati wa uchaguzi mkuu wa Novemba.

Utafiti unaonyesha Biden anaongoza katika majimbo saba katika kinyang’anyiro hicho cha Jumanne, Sanders katika majimbo sita na Seneta Amy Klobuchar akiongoza katika jimbo la nyumbani kwake la Minnesota.

“Itakuwa vigumu sana kuweza kuongeza kuungwa mkono California,” Biden alikiri Jumapili alipokuwa anaongea na kipindi cha ABC News “This Week.” Lakini amesema, “Ninafaraja kwa namna ilivyo katika majimbo mengine, akiongeza kuwa “hata hana uhakika” iwapo atakuwa nyuma ya Sanders katika hisabu ya kura za mkutano mkuu wa Demokratik baada ya kupigwa kura Jumanne.

Joe Biden akifurahia ushindi wake wa kwanza jimboni South Carolina

Biden alitangaza kuwa anaweza kumshinda Rais wa chama cha Republikan Donald Trump katika uchaguzi mkuu wa Novemba na kuwaleta wagombea wa Demokratiki kupata ushindi wa Seneti ambayo hivi sasa inadhibitiwa na Warepublikan.

Majimbo hayo kumi na nne yana theluthi moja ya wajumbe 1991 wanaohitajika kwa mgombea kupata ushindi katika mkutano mkuu wa chama utakaofanyika mjini Milwaukee, jimbo la kati la Wisconsin.

Meya wa zamani wa New York Michael Bloomberg atajitokeza kupigiwa kura kwa mara ya kwanza Jumanne baada ya kuendesha kampeni bila ya kushiriki katika uchaguzi wa majimbo manne ya kwanza.

Mgombea kiti cha rais, meya wa zamani wa New York, Mike Bloomberg.

Sanders alisema alipohojiwa na kituo cha televisheni cha ABC kuwa Biden “alifanya vizuri” uchaguzi wa South Carolina. “Tutaona nini kitatokea Jumanne, lakini tuna nafasi nzuri ya kushinda baadhi ya majimbo makubwa ya Marekani,” alisema.

Baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama cha Demokratiki wameeleza wasiwasi wao juu ya mgombea Sanders, ambaye ametaka kuwepo mfumo wa huduma ya afya unaoendeshwa na serikali na kusitishwa kwa mipango ya bima binafsi ambayo hivi sasa inatumiwa na Wamarekani wengi kusaidia kulipia gharama za matibabu yao.

Viongozi hao wanaeleza wasiwasi wao kuwa kauli hiyo ya itikadii kali za kushoto itamsababisha kutoweza kumshinda Trump anaegombania muhula wake wa pili kubaki White House.