Biden, McCarthy watakutana kujadili ufumbuzi wa ukomo wa deni la serikali ya Marekani

Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mrepublikan Kevin McCarthy ikulu ya White House, Washington.

Rais Joe Biden, Mdemokrat, na Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy watakaa chini Jumanne kujaribu kusonga mbele kuhusu makubaliano  ya kuongeza ukomo wa deni la serikali ya Marekani la dola trilioni 31.4 ili kuepuka janga la  kiuchumi.

Wana muda mfupi kufikia makubaliano. Wizara ya Fedha Jumatatu, imerejea tena onyo lake kwamba inaweza kuwa na upungufu wa fedha kulipa gharama zote ifikapo Juni mosi.

Wachumi wanasema jambo hili litazua kasoro ambayo inaweza kuzua mtikisiko mkubwa wa uchumi.

Warepublican wanaodhibiti Baraza la Wawakilishi kwa wingi wa 222-213 kwa miezi kadhaa wamedai kwamba ongezeko lolote la kiwango cha ukopaji kilichowekwa na serikali kinaweza kuhusishwa na kubana matumizi.

White house imesema mazungumzo hayo yataanza majira ya saa tisa mchana saa za Marekani, Lakini McCarthy Jumatatu alisema anaamini kwamba kuna hatua kadhaa zimefikiwa.