Biden apongeza ushirikiano kati ya Marekani na Angola

Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na rais wa Angola Joao Lourenco Desemba 03,2024. Picha na VOA

Rais Joe Biden wa Marekani ameanza ziara ya siku mbili nchini Angola kwa mazungumzo na mwenyeji wake Rais Joao Lourenco, juu ya ushirikiano wa kibiashara na uchumi.

Biden akiwa kwenye ziara yake ya mwisho ya nje ya nchi na ya kwanza barani Afrika anasisitiza juu ya uwekezaji mkubwa wa Marekani katika nchi hiyo na kanda zima ya Kusini mwa Afrika.

Ziara hii inazingatia zaidi mradi wa kimataifa wa ujenzi wa reli maarufu kama ‘Lobito Rail Corridor’ itakayosafirisha madini na rasilimali ghafi kutoka Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi bandari ya Lobito kusini mwa Angola.

Baada ya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Lourenco, Biden ametembelea Makumbusho ya Kitaifa ya Utumwa mjini Luanda na kuzungumzia juu ya biashara haramu ya binadamu wakati wa karne zilizopita iliyounganisha uchumi wa mataifa yao mawili. Na kuangazia mustakbal wa ushirikiano kwa faida za mataifa yao mawili.

Kesho Jumatano kiongozi huyo wa Marekani atatembelea mji wa Lobito ulioko kilomita 500 kusini mwa Luanda, kiini cha mradi mkubwa utakao gharimu dola bilioni tatu wa Lobito Rail Corridor.

Mradi huo ni mkopo kutoka serikali ya Marekani, Umoja wa Ulaya, Benki za nchi za Afrika na makampuni binafsi kwa lengo la kukarabati njia ya reli itakayoshindana na uwekezaji wa China katika kanda hiyo.