"Rais Biden alizungumza na Rais Volodymyr Zelensky Jumatatu na kuahidi kuendelea kuipatia Ukraine msaada unaohitajika kujilinda, ikiwa ni pamoja na mifumo ya juu ya ulinzi wa anga," ilisema taarifa hiyo.
Rais wa Russia Vladimir Putin, ametishia mashambulizi "makali" zaidi dhidi ya Ukraine, baada ya wimbi kubwa zaidi la mashambulio, tangu vita hivyo kuanza miezi kadhaa iliyopita, kuwaua takriban watu 11 katika kulipiza kisasi, kwa mlipuko ulioharibu daraja kuu linalounganisha Russia na rasi ya Crimea, inayokaliwa na Moscow.
Baada ya kuzungumza na Biden, Zelensky alituma ujumbe wa Twitter akisema; "Ulinzi wa anga kwa sasa ndio kipaumbele cha kwanza katika ushirikiano kati ya Ukraine na Marekani."
Kyiv imesema vikosi vya Russia vimerusha makombora zaidi ya 80 yakilenga miji kadhaa kote nchini Ukraine na kwamba Russia pia imetumia ndege zisizo na rubani za Iran, zilizorushwa kutoka nchi jirani ya Belarus.
Biden Pia alisisitiza kwamba ushirikiano kati ya Marekani na washirika wake, utaendelea kuimarika katika juhudi za kuiwajibisha Russia kwa kile alichokiita “uhalifu wa kivita na ukatili."