Bi Biden ajionea athari za ukame Afrika Mashariki, aahidi 70% ya misaada yote ya kimataifa

Mke wa rais wa Marekani Jill Biden atembelea Kaunti ya Kajiado nchini Kenya, moja ya maeneo yaliyokumbwa na ukame mbaya zaidi.

Mke wa rais wa Marekani, Jill Biden, Jumapili alipata nafasi ya kujionea kwa karibu hali mbaya ya ukame wa kihistoria unaoshuhudiwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bi. Biden alitembelea moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ukame nchini Kenya, katika kaunti ya Kajiado, na kuwasikiliza baadhi ya wanawake wa Kimasai wakieleza jinsi watoto na mifugo wao wanavyokumbwa na njaa.

Alitoa wito kwa nchi zaidi kujiunga na Marekani ili kusaidia kupunguza mateso yanayosababishwa na hali hiyo, akisema kwamba Marekani intoa asili mia 70 ya msaada unaotumwa katika eneo hilo kukabiliana na hali hiyo.

Baadhi ya maeneo ya Pembe ya Afrika yameshuhudia ukosefu wa mvua kwa misimu mitano mfululizo, ikimaanisha hakukuwa na mvua au kiasi cha kutosha kusaidia wakulima na mazao au mifugo yao.

Msimu ujao wa sita wa mvua, unaoanza Machi, unatarajiwa kuwa sawa na hiyo ya awali, au mbaya hata zaidi, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya hali ya hewa.

Biden, ambaye alikuwa katika siku ya mwisho ya ziara ya siku tano barani Afrika, alitembelea kituo cha uhamasishaji katika mji wa Kajiado kinachoendeshwa na World Vision kwa msaada wa UNICEF na Mpango wa Chakula Duniani.

Alizungumza na watu waliowaleta watoto wao kupimwa hali ya utapiamlo na alishiriki katika mazungumzo na kikundi cha wanawake, akiwemo mama wa watoto 10. Watoto pia walielezea msaibu yao.

“Walizungumza jinsi mifugo yao inavyokufa. Ni wazi, unaweza kuona ukame hapa, jinsi ulivyo mbaya,” mke huyo wa rais aliwaambia wanahabari baadaye.

"Chanzo kimoja cha maji hapa kinalisha vijiji 12 na kila kijiji kina takriban watu elfu moja hadi 1,200. Kwa hiyo watu wanakuja kupata maji, wanaleta mifugo yao kupata maji. Lakini kwa bahati mbaya, kwa wengi wao, jinsi maisha yao yanategemea mifugo wao na kwa wengi wao, mifugo wanakufa, kwa hivyo wana wakati mgumu, "alisema.

"Tunahitaji kuwa na nchi zingine kuungana nasi katika juhudi hizi za kimataifa kusaidia watu hawa wa eneo," alisema, akiongeza kuwa ukame unashindana na juhudi za kibinadamu zinazohusiana na vita vya Russia huko Ukraine na tetemeko la ardhi ambalo liliua maelfu ya watu nchini Uturuki na Syria.

"Namaanisha, kuna masilahi mengi yanayoshindana lakini, ni wazi hapa, watu na mifugo wanakufa njaa," alisema.

Jamii ya Wamasai, ambao wengi wao ni wafugaji, inaishi katika kaunti ya Kajiado ambako Biden alitembelea.

Takriban watu milioni 23 nchini Somalia, Ethiopia na Kenya wanakadiriwa kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, ambayo ina maana kwamba hawajui watapata wapi mlo wao ujao, kulingana na jopo kazi linaloangazia usalama wa chakula linachoongozwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Mamlaka ya Maendeleo ya kieneo, IGAD.