Tanzania : Bado wanawake wanaishi kwa hofu kutokana na ubakaji

Tanzania

Tangu kutangazwa kukamatwa kinara wa matukio ya ubakaji na kujeruhi wanawake mkoani Kigoma, Tanzania, inaelezwa kuwa sasa hali imerudi kuwa shwari lakini bado wakazi wangali na hofu licha ya kukamatwa kwa kinara wa matukio hayo.

Wanawake bado wanaa wasiwasi kwamba huenda bado kuna washirika wa uhalifu huo katika jamii ambao hawajakamatwa.

Matukio ya ubakaji na kuwajeruhi wanawake yameripotiwa kutekelezwa na kikundi cha watu kinachojiita Teleza kwa kuvamia makazi ya wanawake wakiwa Uchi na kujipaka mafuta ya kulainishia mitambo yaliyotumika kwa lengo la kutoshikwa pindi anapotaka kukimbia baada ya kutekeleza uhalifu huo

Shukurani Almasi na Dada yake Mayasa Almas ni miongoni mwa wanawake walionusurika katika matukio ya kikundi cha Teleza.

Almasi akiwa anaendelea na kazi katika saluni yake mjini Kigoma, wiki hii ameieleza VOA kumbukumbu za tukio la kutaka kubakwa na kuachiwa kovu kutokana kujeruhi kichwani.

Mayasa Almasi, Mkazi wa Mtaa wa Lusimbi, Kigoma amesema pamoja na kuongeza makomeo na kuimarisha milango kama njia ya kujikinga, bado wakazi wangali na hofu licha ya kukamatwa kwa kinara wa matukio hayo.

Naye Diwani wa kata ya Mwanga Kusini Musa Ibrahim, eneo ambalo limeripotiwa kuwa na kesi nyingi za matukio ya teleza, anasema tangu mwaka 2012 visa vya ubakaji vilivyotekelezwa naTeleza vilisikika japo waathirika waliogopa kutoa taarifa katika vyombo vya usalama wakihofia vitisho vya wahalifu hao.

Kuanzia mwaka 2015 matukio haya yalianza tena na kuongezeka hatua iliyowalizimu kwa kushirikiana na serikali na jeshi la polisi kulivalia njuga na kupelekea watuhumiwa kukamatwa.

Diwani ameeleza kuwa matukio ya aina hii husukumwa zaidi na baadhi ya mienendo ya jamii isiyosawa, Ibrahim anaeleza kuwa uwepo wa vilabu vinavyouza hata Pombe haramu kama Gongo.

Pia amesema vigenge vya wahuni vinapaswa kuchukiliwa hatua za haraka ili kuwapeusha vijana kushawishika kujiingiza katika makundi yasiyofaa na kutoa mwanya kwa wahalifu huku haya yakienda sambamba na rai ya kuimarishwa ulinzi katika maeneo ya Kigoma.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Idd Uwesu, Kigoma, Tanzania