Mjadala wa mabadiliko ya hali ya hewa unatakiwa kuchukua mwelekeo tofauti - Wadau

Rais wa Kenya William Ruto (Katikati) akiandamana na viongozi wengine wa Kiafrika alipotoa hotuba wakati wa hitimishoo la mkutano wa siku tatau wa hali ya hewa barani Afrika uliofanyika mjini Nairobi. Septemba 6, 2023.

Mkutano wa kihistoria wa hali ya hewa barani Afrika ulimalizika Jumatano baada ya viongozi kupitisha azimio linaloangazia uwezo wa bara hilo kama eneo lenye nguvu ya nishati ya kijani, Rais wa Kenya William Ruto alisema.

"Tunasonga mbele na azimio la Nairobi," Ruto alisema, wakati wa kuhitimishwa kwa mkutano huo wa siku tatu, ktika mji mkuu wa Kenya.

Alikuwa ametetea hoja ya kubadilisha mkakati wa mazungumzo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, na kulenga haja ya Afrika kukumbatia nishati safi, wakati bara hilo likikabiliwa na majanga yanayohusiana na hali ya hewa.

"Azimio hili litatumika kama msingi wa msimamo wa pamoja wa Afrika katika mchakato wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani," Ruto alisema.

Wachambuzi wanasema sauti ya pamoja ya nchi za Afrika inaweza kuleta tija kwa msururu wa mikutano muhimu itakayofuata, kwelekea kwa ule wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, utakaoanza mwezi Novemba, wa COP 28, ukiwemo mkutano wa G20 mjini New Delhi wikendi hii.

Bara hilo lenye mataifa 54 liko katika hatari kubwa ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa, lakini mkutano huo ulilenga zaidi wito wa kufungua uwekezaji katika nishati safi.

Ruto alisema mkutano huo ulishuhudia ahadi za ufadhili zenye thamani ya dola bilioni 23 "kwa ukuaji unaotilia maanani usafi wa mazingira, na juhudi za kukabiliana na uchafuziwa mazingira bara zima, alisema.