Mashambulizi hayo yamefanyika Jumamosi asubuhi, majira ya saa kumi alfajiri kwa saa za Somalia, yakilenga kambi za jeshi katika miji ya Barire na Awdhegle kusini mwa Somalia.
Vituo vya uendeshaji vilivyo mstari wa mbele vinavyosimamiwa na jeshi la Somalia ili kulinda madaraja kadhaa yaliyoko kwenye mto Shabelle ambavyo mamlaka inasema ni muhimu katika kuzuia magari yanayo beba vilipuzi kuingia Mogadishu.
Mashambulizi yalianza na gari lenye mabomu ya kujitoa muhanga katika kambi mbili za jeshi, yakifuatiwa na shambulizi la ardhini, maafisa wa mkoa wamesema.
Akiongea na Sauti ya Amerika, Abdulkadir Mohamed Nur Siidi, gavana wa mkoa wa Lower Shabelle, amethibitisha kutokea mashambulizi hayo.
Siidi amesema wapiganaji hao walirusha mabomu katika vijiji jirani vya Sabiid na Anole. Mashambulizi zaidi ya mabomu yameripotiwa katika eneo karibu na mji wa Jannaale.
Katika miaka ya karibuni, jeshi la Kitaifa la Somalia, kwenye operesheni za pamoja na tume ya ulinzi wa amani katika kanda hiyo, vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia, au AMISOM vimeweza kuvikamata tena vijiji hivyo ambavyo hapo awali vilikuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo wa al-Shabaab.
Shambulizi la mabomu siku ya Jumamosi inawezekana ilikuwa ni juhudi ya kusambaratisha uwezekano wa kujizatiti kwa majeshi ya serikali.
Majeshi ya serikali yanaonekana yameweza kuzima shambulizi huko Awdhegle na kulihami daraja kuu linalotumiwa na raia na wanajeshi, lakini kulikuwa na mapigano makali katika mji wa Barire, maafisa wameongeza.
Kikundi cha wanamgambo wa Al-Shabaab kimedai “kuharibu” kituo cha kijeshi cha Barire, afisa mmoja wa mkoa, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu hana ruhusa ya kuongea na vyombo vya habari, amesema Barire imeathiriwa na shambulizi hilo.
Maafisa wawili wamesema wapiganaji hao waliingia katika kambi ya kijeshi ya Barire bila ya kutoa maelezo zaidi. Wapiganaji hao hivi sasa wamefurushwa kutoka Barire, afisa mmoja ameeleza.
Awdhegle na Barire ziko kilomita 75 na kilomita 60 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu
Televisheni ya taifa inayodhibitiwa na serikali imeripoti kuwa majeshi ya serikali “yamezima” mashambulizi ya al-Shabaab huko Awdhegle na Barire. Wapiganaji wamepata hasara kubwa, kwa mujibu wa matangazo ya kituo cha televisheni cha serikali.
Mkuu wa Majeshi ya Somalia Brigedia Jenerali Odawaa Yusuf Rageh amesema “Majeshi ya Somalia yamewauwa darzeni ya wanamgambo magaidi wakiwemo viongozi wao baada ya al-Shabaab kushambulia vituo vya SNA [Jeshi la Kitaifa la Somalia] huko Awdhegle na Barire katika mkoa wa Lower Shabelle,” kupitia ujumbe wa Twitter uliotangazwa na chombo cha habari cha serikali, Kituo cha Televisheni cha Taifa cha Somalia.