Afrika Kusini huenda ikasuluhisha vita vya Russia na Ukraine

Mwanajeshi wa Ukrainie akionyesha alama ya 'V' kama ishara ya ushindi , wakati akipokea mafunzo ya mizinga ya kivita ya Leopard 2, tarehe Machi 13, 2023. Picha na OSCAR DEL POZO / AFP.

Ubelgiji siku ya Alhamisi imeitaka Afrika Kusini kutumia uhusiano wake na Russia kusaidia kumaliza vita nchini Ukraine, matamshi hayo yalitolewa wakati wa ziara ya Mfalme wa Ubelgiji mjini Pretoria.

"Kwa kuzingatia uhusiano wako wenye nguvu wa kihistoria na Russia, tutafurahi kama utafikiria kutumia njia zako za mawasiliano ili kusukuma mbele suala la amani" Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Hadja Lahbib alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Pretoria.

Lahbibi amefuatana na Mfalme Philippe wa Ubelgiji na Malkia Mathilde ambao wako katika ziara yao ya kwanza ya siku tano nchini Afrika Kusini.

"Siku zote tumekuwa tukiiona Afrika Kusini kama mshirika mkuu wa amani na utetezi wa haki za binadamu," Lahbib alisema.

Rais Cyril Ramaphosa alijibu kwa kusema Pretoria inaendelea "kutumia njia walizonazo na Russia...kuzungumza jinsi ya kuumaliza mzozo huo".

Mamlaka yenye nguvu katika bara la Africa imekataa kulaani uvamizi wa Ukraine ambao kwa kiasi kikubwa umesababisha Moscow kutengwa katika jukwaa la kimataifa, mamlaka hiyo imesema inataka kutoegemea upande wowote na inapendelea mazungumzo yatakayomaliza vita.

Wito huo umekuja baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati ya kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin Ijumaa iliyopita.

Hati hiyo ya ICC " imeweka wazi kuwa jambo hilo linatia wasiwasi" Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor, aliviambia vyombo vya habari pembeni ya ziara hiyo kwenye makao makuu ya serikali mjini Pretoria.

Afŕika Kusini inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa BRICS – jumuiya ambayo inashirikishanchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amethibitisha kuwa Putin amealikwa huhudhuria mkutano huo.

Afrika Kusini ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, kwa hiyo itatarajiwa kutekeleza agizo la kukamatwa kwa Putin iwapo ataingia nchini humo.

Uhusiano wa Afrika Kusini na Russia ulianza miongo kadhaa iliyopita wakati Kremlin ilipokiunga mkono chama tawala cha African National Congress katika mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi.

###

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP