Rais Cyril Ramaphosa ametoa tangazo hilo alipokuwa katika ziara ya kiserikali nchini Qatar, ambako amesema amezungumza na mtawala wa taifa hilo kuhusu hali ya kibinadamu inayozidi kuwa mbaya huko Gaza.
"Sote tumechukizwa sana na kile kinachotokea hivi sasa huko Gaza, ambayo imegeuka kuwa kambi ya mateso ambako mauaji ya halaiki yanafanyika," alisema.
Ramaphosa alisema Afrika Kusini haikuunga mkono hatua zilizochukuliwa na Hamas wakati kundi hilo lilipofanya shambulio baya dhidi ya Israel mwezi uliopita na kuua zaidi ya watu 1,200 na kuwachukua mateka 240.
Hata hivyo, ameikosoa Israel kwa hatua ilizochukua, akisema watu "wanakufa kama nzi" katika hospitali za Gaza zilizozingirwa.
"Kama Afrika Kusini, kwa hiyo, pamoja na nchi nyingine nyingi duniani, tumeona inafaa kuliwasilisha suala linaloihusu serikali nzima ya Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu," alisema.
Alipotafutwa na VOA, balozi wa Israel Eliav Belotsercovsky hakutoa maoni yoyote.
Israel daima imekuwa ikisisitiza kwamba inachukua hatua katika kujilinda. Mapema wiki hii, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Israel ilikuwa inafanya "juhudi zisizo za kawaida" kupunguza vifo vya raia.
Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi duniani zinazounga mkono zaidi Wapalestina. Chama tawala cha African National Congress mara nyingi kimekuwa kikiweka kile kinachosemekana kuwa ni uwiano kati ya mapambano ya Waafrika Kusini Weusi dhidi ya utawala wa kibaguzi na hali iliyoko Mashariki ya Kati.