Afrika Kusini yachukuwa hatua kuzuia mashambulizi ya kibaguzi

Wezi wakiiba katika duka lilioko mtaa wa Germiston, mashariki ya Johannesburg, Afrika Kusini, Jumanne Sept. 3, 2019. Wezi hao walikuwa wanakusudia kuiba katika maduka ya wafanyabiashara wageni na polisi walitumia risasi za mpira kuwatawanya wezi

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amewaambia maafisa na viongozi wa biashara kwamba serikali yake inachukuwa kila hatua kumaliza mashambulizi yanayoendelea dhidi ya wageni, suala lililoghubika mkutano wa kiuchumi unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara barani Afrika.

Polisi wamewakamata watu kadhaa na kuripoti vifo vya watu kufuatia mashambulizi hayo, katika miji ya Johannesburg na Pritoria.

Makundi ya watu wa Afrika Kusini yamekuwa yakishambulia maduka ya biashara yanayomilikiwa na raia kutoka nchi nyingine za Afrika.

Hakuna taarifa maalum imetolewa kueleza sababu za kutokea mashambulizi hayo lakini wachambuzi wanasema yamechochewa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, na ukosefu wa fursa za kiuchumi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Palamagamba Kabudi amesema serikali ya Tanzania haitajiingiza katika malumbano na serikali ya nchi hiyo kutokana na vurugu hizo, bali inaamini kuwa tamko lililotolewa na Rais Cyril Ramaphosa la kukemea vurugu hizo linatosha kusitisha mihemko yeyote ya baadhi ya wananchi hao.

Amesema kwamba Tanzania itaendelea kusimamia uhusiano mwema na wa kindugu baina ya nchi hizo mbili huku akifafanua kuwa vurugu hizo nchini Afrika Kusini zinatokana na mapambano ya kihistoria kati ya wananchi wa nchi hiyo weusi waliobaguliwa kwa muda mrefu hali iliyowasababisha ukosefu wa elimu ya kuwawezesha kuajiriwa.

Mapema Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC Dkt. Stergomena Lawrence Tax alikaririwa akilaani matukio hayo ya kibaguzi yaliyotokea nchini Afrika Kusini

Katika vurugu hizo inaripotiwa magenge ya raia wa Afrika Kusini wanavamia biashara zinazomilikiwa na wageni katika maeneo tofauti ya Afrika Kusini, kupora mali na kuchoma magari ya wageni.

Kufuatia muendelezo wa vurugu za chuki dhidi ya raia wa nchi za kigeni za Kiafrika, Kenya inaeleza kuwa inafuatilia matukio hayo kwa ukaribu mno.

Serikali ya Kenya imeeleza kuwa raia wake wawili wamelengwa katika ghasia hizo zinazolenga wahamiaji nchini humo na kueleza kuwa huo si mkondo mataifa ya Afrika unafaa kufuata.

Maeneo kadhaa ya Afrika Kusini kama vile Pretoria, Cape Town, Johannesburg na Alexandria yameripotiwa kuwa vitovu vya vurugu hizo zilizosababisha maafa na uharibifu wa mali yenye thamani kubwa.

Imetayarishwa na waandishi wetu, Kenya, Tanzania, Washington, DC.