Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa amelaani wizi wa ngawira uliosamba mnamo siku kadhaa na mashambulizi ya moto dhidi ya maduka ya wafanyabiashara wa kigeni kote Johannesburg pamoja na mji mkuu Pretoria akieleza ghasia hizi hazikubaliki kabisa.
Rais Ramaphosa alisema kwenye taarifa ya video iliyotangazwa Jumanne kwamba wako katika nchi ambayo haikubali kabisa chuki dhidi ya wageni. Alisema hawaruhusu na wala hawastahmili mashambulizi wanayofanyiwa watu kutoka mataifa mengine ya kiafrika.
Polisi waliongeza usalama kwenye mitaa yote ya Johannesburg na Pretoria wakati ghasia zinaendelea kwa siku ya tatu. Polisi wamewakamata zaidi ya watu 90 katika maeneo matano yaliyoathiriwa na ghasia hizo ambako wamevunja na kupora mali kutoka maduka hayo ambayo yanamilikiwa na wageni ambao wanaogopa kurudi katika maduka yao.