Kulingana na mwakilisi wa shirika la kiraia Ricardo Rupande, wapiganaji wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) walianza mashambulio hayo mapya wakati wa magharibi, kwenye kijiji cha Bukokoma, kilichopo wilaya ya Beni, jimbo la Kivu Kaskazini.
Kundi la Islamic State linadai ADF ndio mshirika wake wa Afrika ya kati. Kundi hilo ni moja kati ya wanamgambo wanaosababisha mauwaji ya kikatili huko mashariki ya Congo wakituhumiwa kwa kuwachinja maelfu ya raia.
Katanga Matete, afisa wa utawala wa tarafa ya Bukokoma, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanamgambo hao "walikuwa wakifungua milango na kuwakata watu vichwa kwa kutumia sululu na mapanga."
Amesema watu kumi na wawili waliuliwa.
Afisa wa shirika la Msalaba Mwekundu, Albert Ndungo, alithibitisha kuuliwa kwa 12 "kwa panga zilizochongwa," wakiwemo wanawake wanne na watoto wanne.
Ghasia za Alhamisi zinafuatia shambulizi linalofanana na hilo lililotokea wiki iliyopita katika wilaya ya Beni ambako watu tisa waliuwawa.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.